Chadema wakemea viongozi kutumia madaraka vibaya


Dalila Sharif

BARAZA la Vijana Chadema (BAVICHA) limekemea baadhi ya viongozi wanaotumia madaraka vibaya kwa kuwakamata viongozi wa chama hicho kwa kutumia nguvu za madaraka yao.

Pia Baraza limesema liko tayari kumfungulia kesi Mkuu wa Wilaya ya Ubongo, Kisare Makori kwa kukiuka na kuingilia muhimili wa mamlaka husika katika kumwamuru Meya wa Ubongo, Boniface Jacob akamatwe bila sababu za msingi.

Kauli hiyo ilitolewa  Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa Baraza hilo, Potrabas Katambi akisema ukamataji viongozi wa chama hicho umeendelea kukua kwa kasi, huku baadhi ya viongozi wa chama tawala wakitumia madaraka yao kunyanyasa viongozi wa vyama pinzani.

Alisema hali hiyo inakiuka taratibu za mamlaka husika kufanya kazi zake na kuingilia viongozi wenye majukumu yao mengine kwa kutumia sheria vibaya.

“DC wa Ubungo ametumia mamlaka vibaya kuamrisha kumkamata Meya wa Jimbo hilo kwa kudhaniwa kuwa anafanya mkutano jambo ambalo si kweli,” alisema Katambi.

Alisema vitendo vya wakuu wa wilaya na mikoa kutumia madaraka yao   kukamata watu ni uonevu wa hali ya juu, hali ambayo haiwezi kufumbiwa macho na chama chake.

Aidha, amewataka viongozi kutoingilia madaraka ya chombo husika na kulitaka Jeshi la Polisi kusimamia wenye haki na si kupewa amri na baadhi ya viongozi ili kukomoa watu.

“Mchezo huu tunaomba usitishwe mara moja, kwa sababu viongozi wa namna hii wanatafuta kiki za kupata umaarufu na si kutumikia jamii katika kutatua changamoto zao,” alisema Katambi.

Alisema upinzani si vita, bali ni kuibua changamoto za hamasa kwa chama tawala katika kufanya kazi kwa bidii, hivyo kutumiwa vibaya vyama vya upinzani ni upotoshaji wa amani.

Hata hivyo, tukio la kukamatwa kwa Meya huyo lilitokea Jumatatu saa sita mchana makao makuu ya wilaya hiyo yaliyo Kibamba baada ya kuzuia msafara huo, ulioshirikisha viongozi wa Chadema akiwamo Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye na viongozi wengine wa Ubungo na Kanda ya Pwani.

Pia alimwomba Rais John Magufuli, kusimamia vema suala la mchanga wa madini (makinikia) na Akaunti ya Escrow kwa kuwataka viongozi waliohusika na hayo kuchukuliwa hatua mara moja.   
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo