Mwanasheria TBS afutiwa kesi ya makazi


Grace Gurisha

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam imemfutia kesi ya kuishi nchini bila kibali Mwanasheria Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Baptister Bitaho (54).

Hata hivyo, baada ya mshitakiwa huyo kuachwa huru jana alikamatwa tena na yupo Idara ya Uhamiaji akihojiwa.

Mahakama hiyo ilifikia uamuzi huo, baada ya Mwendesha Mashitaka wa Uhamiaji, Method Kagoma kuiomba Mahakama imfutie kesi chini ya kifungu cha 98(a) cha sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA).

Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa alikubaliana na maombi hayo na kuifuta kesi hiyo, ambayo mshitakiwa alikuwa anakabiliwa na mashitaka matatu.

Awali, Mwendesha Mashitaka wa Uhamiaji, Novatus Mlay alidai kuwa Mei 19 maeneo ya Kinondoni katika ofisi ya Uhamiaji, Bitaho akiwa raia wa Burundi, alikutwa nchini bila kibali cha kumwezesha kuishi nchini.

Alidaiwa kuwa Bitaho siku hiyo alikutwa akifanya kazi kama Mwanasheria Mkuu wa TBS bila kibali kinachomruhusu kufanya kazi nchini.

Alidai kuwa Julai 6, 2011 katika ofisi ya Uhamiaji ya Mkoa wa Dar es Salaam wilayani Ilala, mshitakiwa huyo akiwa raia wa Burundi, alitoa taarifa za uongo kuhusu maelezo yake binafsi, wakati akijaza fomu ya kuomba hati ya kusafiria namba CT (5)(Ai).

Wakili Mlay aliongeza kuwa kitendo hicho cha kutoa taarifa za uongo kilimwezesha Bitaho kupata hati ya kusafiria ya Tanzania yenye namba AB 474856 huku akijua kufanya hivyo ni kinyume cha sheria za nchi.

Baada ya kusomewa mashitaka hayo, alikana na upande wa mashitaka kudai kuwa upelelezi bado haujakamilika na alikuwa nje kwa dhamana baada ya kukamilisha masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika, ambao kila mmoja alisaini dhamana ya Sh milioni 20.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo