Kumekucha CUF


*Bodi ya wadhamini yatambuliwa rasmi na Rita
*Ni iliyo upande wa Mwenyekiti Prof. Lipumba

Celina Mathew

Lipumba na Maalim Seif
WAKALA wa Ufilisi na Udhamini (Rita), umeidhinisha Bodi Mpya ya Wadhamini ya CUF, huku chama hicho kikitarajia kufuta kesi zilizo mahakamani zilizofunguliwa na Bodi iliyopita ikiwamo ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi na viongozi wake wengine ikieleza kuwa mgogoro uliokuwapo umemalizika.

Aidha, CUF chini ya uenyekiti wa Profesa Ibrahim Lipumba, imemtaka Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Sharrif Hamad kusamehe yaliyopita na badala yake aende ofisi ya makao makuu Buguruni kuendelea na kazi za kukijenga upya chama.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu wa Bodi hiyo, Thomas Malima alisema usajili wa Bodi hiyo ni kwa mujibu wa sheria ya udhamini na ya muunganisho wa wadhamini sura ya 318 toleo la 2002.

Alisema kwa mujibu wa sheria namba tano ya mwaka 1992 ya usajili wa vyama vya siasa, inataka kila chama kilichosajiliwa kuwa na Bodi ya Wadhamini iliyosajiliwa na Rita na inaishi kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi.

Kwa mujibu wa Katiba ya CUF ya mwaka 1992 toleo la 2014 ibara ya 98(1) Bodi ya Wadhamini ya CUF itadumu kwa miaka mitano kisha itateuliwa nyingine kwa kutumia sheria ya muunganisho wa wadhamini sura ya 318, toleo la 2002

Aliongeza kuwa mjumbe wa Bodi hiyo anaweza kuteuliwa tena na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa baada ya muda wake kumalizika.

Alisema Bodi hiyo kwa kawaida huundwa na wajumbe tisa ambapo watano kati yao lazima watoke Tanzania Bara na wajumbe wanne Zanzibar ambapo mmoja anapaswa kuwa mwanamke na hiyo ni kwa mujibu wa Katiba ya Chama hicho ibara ya 98 (2).

Alisema majukumu ya kikatiba ya Bodi hiyo ni kudhamini fedha na mali za chama na madeni, pia ndiyo yenye mamlaka ya kushitaki au kushitakiwa kwa niaba ya chama.

Malima alifafanua, kuwa upembuzi yakinifu uliofanywa na Rita, ulibaini uhalali wa mabadiliko ya Bodi hiyo kuwa yamekidhi matakwa ya Katiba ya CUF ambapo Juni 12 walikiandikia chama barua.

“Tuliandikiwa barua rasmi ya kutufahamisha kuwa wamejiridhisha kwamba wadhamini walioteuliwa walikidhi vigezo vya udhamini na hivyo kuwasajili rasmi,” alisema.

Alisema baada ya kupokea barua hiyo ya Rita, wao Bodi ya Wadhamini walikaa na kuazimia kuwa yeye aandike barua kwa benki zote zenye akaunti za CUF nchini, kuzitaka ziruhusu miamala ya kuweka na kutoa fedha za chama kwa kuwa ndiyo halali inayotambuliwa na Rita.

Aliongeza kuwa Bodi hiyo imeteua watia saini wapya wa akaunti zote za CUF ngazi ya Taifa na imethibitisha akaunti ya CUF ya benki ya NMB tawi la Temeke kuwa akaunti ya wadhamini ngazi ya Taifa.

Alitoa hadhari kwa wanachama wanaojiita Kamati ya Uongozi ya Taifa kuacha mara moja na wakisikika wanajivika nyadhifa hizo watachukuliwa hatua na Bodi ya Wadhamini.

Kesi

Katika hatua nyingine, chama hicho kinatarajia kufuta kesi zilizofunguliwa kwenye mahakama mbalimbali nchini na iliyokuwa Bodi ya Wadhamini ya CUF dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Mwenyekiti wa Chama, Kaimu Katibu Mkuu na viongozi wengine.

“Ijumaa (kesho) tutaanza kufuta kesi mbili zilizofunguliwa na Bodi iliyopita pia tumeondoa mawakili wote wa mwanzo kwenye mahakama zote, tumeweka wapya na sasa wanaendelea na kazi wakifuatilia masuala mbalimbali yakiwamo ya kesi za wizi wa ruzuku za chama na inayomhusu Msajili,” alisema.

Mkurugenzi wa Habari wa CUF, Abdul Kambaya alisema chama hicho kimeteseka sana na mgogoro uliokuwepo, lakini kwa kuwa sasa Bodi mpya imepatikana changamoto hiyo itakwisha.

“Tumeteseka sana, wanachama wameumia kujenga chama, lakini wenzetu wenye uchu wa madaraka wakakitupa na kuunga mkono mafisadi, kwa sasa CUF tuko tayari kuanza upya kuliko kuendelea kubomolewa,” alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo