Baba amzoeza mwanawe kaburi


SICHUAN, China

Zhang Liyong
BABA aliyekata tamaa mkazi wa China vijijini amechimba kaburi kwa ajili ya binti yake anayeugua ili “kumwandaa kwa kifo chake”.

Zhang Liyong, mkulima wa jimbo la Sichuan, ametumia akiba yake yote kumtibu mwanawe huyo, ambaye alizaliwa akiwa na tatizo kubwa la damu.

Baba huyo alisema amekuwa akimpeleka binti yake huyo mwenye miaka miwili kaburini hapo kucheza na kupumzika kila siku ili “alizoee eneo hilo ambalo anatarajiwa kuzikwa.”

Video iliyotumwa na kampuni ya Pear Video imeonesha tukio hilo linalogusa nyoyo za watu, lililotokea jijini Neijiang, Kusini Magharibi mwa China.

Kwenye video hiyo, baba anaonekana amelala ndani ya kaburi hilo huku amempakata binti yake huyo, Zhang Xinlei.

Xinlei aligundulika na ugonjwa ujulikanao kama thalassemia, ugonjwa wa kurithi unaohusu damu, akiwa na umri wa miezi miwili.

Zhang na familia yake walitumia zaidi ya yuan 100,000 (pauni 11,490) kumtibu Xinlei, lakini wakashindwa kuendelea kumudu gharama hizo za matibabu.

“Tulikopa fedha kutoka kwa watu wengi, lakini kwa sasa hawako tayari tena kutukopesha,” Zhang alisema.

Wawili hao walifikiria kuzaa mtoto mwingine ili wapate damu ya kiunga mwana ili itumike kumwokoa Xinlei. Hata hivyo, waligundua kuwa hatua hiyo isingewezekana baada ya mke wa Zhang kupata ujauzito. 

“Tumebanwa. Hatuna chaguo lingine,” Deng Min ambaye ni mama wa binti huyo alisema. Waliamua kukata tamaa ya tiba na kujielekeza kwenye maandalizi ya kifo cha Xinlei.

“Hili ndilo wazo pekee nililobaki nalo – kumleta kucheza hapa. Hapa ndipo mahali atakapopumzika milele kwa amani. Ninachoweza kufanya ni kuja naye hapa kila siku,” baba huyo, Zhang alisema.

Anatumaini kwamba Xinlei atalizoea kaburi hilo na hivyo hatakuwa na hofu siku ikiwadia.

Thalassemia ni ugonjwa wa damu wa kurithi. Kwa mujibu wa NHS, watu wenye hali hiyo hutengeneza kidogo au hawatengenezi kabisa himoglobini, ambayo hutumiwa na seli nyekundu za damu kusafirisha hewa ya oksijeni mwilini.

Watu wenye tatizo hilo huhitaji tiba ya maisha yote kwa kuwekwa damu nyingine kila mara au tiba ya Chelation.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo