Ziara ya Magufuli ni ya kukomboa Watanzania


Rais Magufuli ziarani
RAIS John Magufuli anafanya ziara ya siku tatu mkoani Pwani, ambako pamoja na kuzungumza na wananchi wa mkoa huo, anazindua miradi mbalimbali ya viwanda vitano na mradi wa upanuzi wa mtambo wa maji wa Ruvu Juu na ulazaji mabomba kutoka Mlandizi hadi Dar es Salaam.

Uamuzi wa Rais kufanya ziara hiyo kama sehemu ya utekelezaji Ilani ya Uchaguzi ya CCM, ni wa kutia moyo na hakika unaamsha ari ya wananchi kuona jinsi kiongozi wao alivyo karibu nao katika jitihada zake za kuwatafutia maendeleo kwa kuwaondolea adha na kero mbalimbali.

Uzinduzi wa viwanda hivyo, unaweka uhakika wa wananchi wa maeneo hayo na jirani kupata ajira lakini pia wananchi wa Pwani na Dar es Salaam wanapata maji safi na salama kwa muda wote na kuwatua ndoo wanawake.

Rais Magufuli katika ziara hiyo, anazindua kiwanda cha vifungashio cha Global Packaging Ltd, cha kuunganisha trekta cha UrsusTamco Ltd, cha chuma cha Kilwa Steel Group, cha matunda cha Elven Argic na cha vinywaji baridi cha Sayona Fruits.

Wakati anaanza ziara yake wilayani Kibaha juzi, Rais alitumia fursa hiyo kuwaonya wananchi wa Kibiti, Mkuranga na Rufiji dhidi ya watu wachache wanaovuruga amani katika maeneo yao huku wakiwafahamu bila kuchukua hatua.

Alisema mazingira yaliyo kwenye maeneo hayo yanazuia wawekezaji kwenda kuwekeza kwa kujenga viwanda vyao, akiwahoji kuwa nani atakwenda kuwekeza viwanda maeneo ambako watu wanauana? Lakini akaahidi kukabiliana na waovu hao.

Rais alitoa onyo hilo kutokana na kwamba katika maeneo hayo kumetokea mauaji ya Watanzania 36 wakiwamo viongozi wa siasa, Serikali na askari wa Jeshi la Polisi.

Sisi na Watanzania wanaoitakia mema nchi hii, tunaamini kwamba Rais Magufuli ana nia ya dhati ya kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa mahali salama na rafiki ambapo maendeleo yanaweza yakafanyika na kuonekana.

Kwa maana hiyo, ahadi yake ya kukabiliana na wavunjifu wa amani Pwani na maeneo mengine nchini ni ya dhati na ambayo inastahili kuungwa mkono na kila Mtanzania mwema, lakini pia kulinda miundombinu hiyo ambayo anaizindua.

Tunapenda pia kumsaidia Rais kutoa mwito kwa wamiliki na wafanyakazi wa miradi hiyo, kuhakikisha wanaitunza ili nao iwatunze, kwa kuacha kuiba spea za mitambo na bidhaa zinazozalishwa au kwa kifupi kuacha kuihujumu.

Hiyo ni hatua ya kwanza ya kuelekea katika kuwa na Tanzania ya Viwanda na ya uchumi wa kati, kamwe hatutafika huko endapo tutashindwa kuzienzi nguvu na dhamira ya dhati ya Rais Magufuli katika kuwaletea Watanzania maendeleo.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo