Lowassa atikiswa


Celina Mathew

Edward Lowassa
WAZIRI Mkuu wa zamani ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa amehojiwa kwa zaidi ya saa nne na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai
(DCI), Robert Boaz.

Sababu za DCI kumhoji Lowassa ni baada ya kudaiwa kuwa ametoa kauli ya uchochezi baada ya kutaka Rais John Magufuli kutafakari hatima ya masheikh wa Jumuia ya Uamsho na mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumuki) maarufu ëUamshoí wanaosota gerezani kwa miaka minne sasa bila kesi yao kuamuliwa.

Hivyo kutokana na kauli hiyo ambayo Lowassa aliitoa siku za karibuni, juzi Jeshi la Polisi Makao Makuu lilitoa taarifa kuwa anahitajika kwa DCI kwa ajili ya kuhojiwa na jana alitii agizo hilo na kwenda kuhojiwa.

Akizungumza jana baada ya Lowassa kuhojiwa na DCI, Wakili wake, Peter Kibatala alisema Waziri Mkuu huyo wa zamani alipomaliza kuhojiwa alijidhamini mwenyewe ila kesho atatakiwa kwenda tena kwa ajili ya mahojiano mengine.

Wakili Kibatala alisema kwa mujibu wa mahojiano hayo, Lowassa anadaiwa kutoa matamshi hayo siku tatu zilizopita katika futari iliyoandaliwa na Mbunge wa Ukonga jijini Dar es Salaam, Mwita Waitara (Chadema).

Lowassa ataja kiini cha kuhojiwa Akizungumza na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali nyumbani kwake Masaki jijini Dar es Salaam, Lowassa alisema ameitwa kuhojiwa Polisi kutokana na hotuba yake aliyotoa kwenye futari.

“Watu wametafsiri ni uchochezi. Nimewajibu na wanaendelea kutafakari. Tunakutana tena Alhamisi (kesho) saa sita mchana. Siwezi kueleza tumezungumza nini. Nawataka tu watu kuwa watulivu katika kipindi hiki,” alisema Lowassa.

Hata hivyo, Lowassa ambaye hakutaka kujibu baadhi ya maswali kutokana na kile alichokiita kuingilia mahojiano hayo aliwashukuru wanahabari kwa kuandika habari mbalimbali za kuisaidia nchi huku akifafanua kuhojiwa si jambo baya na kutaka hatua stahiki zizingatiwe.

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk.Vicent Mashinji alipoulizwa kuhusu kitendo cha Lowassa kuhojiwa, alisema alichokisema Lowassa kuhusu Uamsho wanaungana nacho kwani ni kweli mashekhe hao wamekaa rumande kwa muda mrefu.

Dk. Mashinji ambaye alionekana akizuiwa kwa nyakati tofauti na Lowassa kutozungumza kwa undani suala hilo, alisema hata Katiba ya nchi inampa mshtakiwa uhuru hadi pale mashtaka dhidi yake yatakapothibitishwa.

Kauli ya Lowassa katika futari Lowassa, alisema ni jambo la fedheha kwa nchi iliyopata uhuru zaidi ya miaka 50 kuwaweka mahabusu viongozi wa dini (mashekhe) muda mrefu kiasi hicho bila kesi kusikilizwa mahakamani.

Kwa kukumbusha tu mashekhe hao awali walikuwa wamefunguliwa kesi ya ugaidi, ambayo ilikuwa ikiendeshwa Mahakama Kuu ya Zanzibar na baadaye kuhamishiwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam inakoendelea hadi sasa.

Hivyo Lowassa alisema iwapo mashekhe hao wamefanya makosa wapelekwe mahakamani ili haki itendeke lakini kuendelea kuwashikilia ni fedheha kubwa kwa Taifa.

Lowassa alisema kama ambavyo Rais John Magufuli ametekeleza ahadi ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kwa kuunda tume mbili za kushughulikia madini ya dhahabu, hana budi kutekeleza na ahadi yake (Lowassa) kuwatoa kizuizini mashekhe hao wa Uamsho.

Uamsho mwaka 2011 Mwaka 2011 viongozi hao wa Uamsho wakiongozwa na Sheikh Farid Hadi Ahmed (41) walikamatwa na kufunguliwa mashitaka kwa tuhuma za kusababisha uharibifu wa mali za watu na Serikali na kuhatarisha usalama wa taifa.

Mara kadhaa wamekuwa wakifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu chini ya ulinzi mkali wa askari wenye silaha za moto kutokana na kushitakiwa kwa tuhuma za ugaidi.

Mbali na kina Farid, kesi za ugaidi zaidi ya 20 zinaendelea mahakamani zikiwahusisha washtakiwa zaidi ya 60.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo