Sababu 3 upinzani kuikataa Bajeti ya JPM


Fidelis Butahe

Rais John Magufuli (katikati)
WAKATI wabunge leo wakitarajiwa kupiga kura ya wazi kupitisha Bajeti ya mwaka 2017/18 ya Sh trilioni 31.7, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, Freeman Mbowe ametaja sababu tatu za kuipigia kura ya hapana bajeti hiyo ya pili ya Rais John Magufuli.

Mwenyekiti huyo wa Chadema amesema baada ya siku nane mfululizo za kujadili mapendekezo na makadirio hayo ya Serikali, bajeti hiyo itapitishwa kwa mbwembwe na wabunge wa CCM, lakini vyama vya upinzani vitaipinga kwa kile alichokiiita; “haijalenga kumkomboa Mtanzania masikini.”

Akizungumza na gazeti hili jana, Mbowe alitaja sababu tatu za wapinzani kuikataa bajeti hiyo kuwa ni; kuongezeka kwa kiwango cha bajeti kutoendana na maisha halisi ya wananchi, kuongezeka kwa deni la Taifa na kutokuwa na jibu na suluhisho kwa wananchi juu ya kupanda kwa gharama za maisha.

Baada ya wabunge kupitisha bajeti kwa kura ya wazi, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango atawasilisha Muswada wa Sheria ya Fedha kwa mwaka 2017.18 utakaowezesha kutumika kwa fedha hizo.

Mbowe ambaye ni mbunge wa Hai alitolea mfano utekelezaji wa asilimia 38 ya bajeti ya mwaka 2016/17 ya Sh trilioni 29 na kuhoji fedha zitakapopatikana kutekeleza bajeti ya Sh trilioni 31.7 walati vyanzo vya mapato vikiwa havieleweki.

Hata hivyo, Serikali ilieleza sababu tatu za kutotekelezwa kwa bajeti hiyo kuwa ni; mwenendo wa upatikanaji wa fedha, upatikanaji wa maeneo ya uwekezaji na matayarisho hafifu ya miradi ambayo baadhi imeonekana ama ipitiwe au majadiliano yaanze upya ili kulinda masilahi ya Taifa.

Bajeti hiyo ya Sh31.7 trilioni iliyowasilishwa bungeni na Dk Mpango takribani siku 10 zilizopita imeweka unafuu ambao utasisimua shughuli za kiuchumi baada ya kufanya marekebisho ya kodi mbalimbali.

Baadhi ya maeneo yaliyowekewa unafuu ni punguzo la kodi ya usajili wa magari, kufuta Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye bidhaa za mtaji, huduma za usafirishaji bidhaa kwenda nje, vyakula vya mifumo na mayai ya kutotoresha vifaranga.

Lakini machungu yatakuwepo katika mafuta ya petroli, pombe aina ya bia na mvinyo wa nje ambazo kama ilivyo kwa miaka mingine, zimekuwa zikiongezwa ushuru.

Wakati Serikali ikija na vyanzo vya mapato vilivyozoeleka, upinzani waliwasilisha bajeti mbadala na kutaja vyanzo vipya vya mapato ambavyo ni; mapato yatokanayo na uvuvi katika bahari kuu, madini ya vito kutokana leseni na kodi na malipo kulingana na kipato (P.A.Y.E).

Nyingine ni kupunguza misamaha ya kodi kwa asilimia moja ya Pato la Taifa, amana za fedha za kigeni (eurobond), mapato kutoka sekta ya utalii na mapato katika sekta ya michezo ya kubahatisha ambavyo kwa ujumla wake alisema vingeliingizia Taifa Sh30 trilioni.

Sababu tatu

“Tunaona kama tunapanua wigo mpana wa bajeti na matumizi makubwa ya Serikali lakini hauendani na kuondoa umasikini wa Watanzania wa kawaida,” alisema Mbowe na kuongeza:

“Kukua kwetu kwa Pato la Taifa (GDP) hakuakisi maisha ya wananchi wa kawaida bali kundi la watu wachache ambao wako katika sekta muhimu za fedha, ujenzi na mawasiliano.”

Alisema wakati sekta hizo zikimulikwa zaidi, sekta nyingine kama kilimo, uvuvi na ufugaji ambazo zimeajili asilimia 70 ya Watanzania hazijapwa kipaumbele katika Mpango wa Serikali wa Miaka Mitano.

Alihoji: “Matokeo yake fedha tunapeleka kwenye ujenzi wa reli na ununuaji wa ndege. Hata shirika la ndege la Tanzania linatengewa fedha nyingi kuliko sekta ya kilimo?”

Mbowe ambaye alisema bajeti hiyo huenda ikawa ya kiini macho zaidi kuliko zote alizozishuhudia tangu awe mbunge miaka 15 iliyopita, alieleza kwamba wapinzani wanaipinga kwa sababu haijaweka msukumo katika maeneo yanayoweza kunyanyua uchumi wa wananchi.

Kuhusu deni la Taifa ambalo limefikia Sh trilioni 42.45, Mbowe alisema: “Katika mwaka wa fedha unaokwisha deni la Taifa lilitumia asilimia 65 ya makusanyo yote ya kodi yatokanayo na TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) kukosekana fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo.”

“Pamoja na hili Serikali inasema deni linahimilika na wanaendelea kukopa. Katika mwaka wa fedha unaomalizika Serikali imekopa Sh trilioni 9 kutoka ndani na nje ya nchi,”alisema.

Kwa mujibu wa Mbowe, katika mwaka ujao wa fedha (2017/18), fedha itakayolipia deni la Taifa ni kubwa kuliko iliyotumika kwenye bajeti ya 2016/17.

“Ina maana uwezo wa Tanzania kukusanya na kupanua mapato unapungua na matumizi ya kuhimili deni la Taifa yanaendelea kuwa makubwa,” alisema Mbowe.

Alisema kwa mantiki hiyo fedha zitakazokwenda katika miradi ya maendeleo zitazidi kuwa pungufu ya asilimia 34.6 ya zilizotengwa katika bajeti ya mwaka 2016/17.

“Deni la Taifa linahitaji mkakati maalum wa kuzuia kukua kwake maana tumeshathibitisha deni hili linatumia makusanyo mengi ya TRA, tunalazimika kukopa fedha ili kuiendesha Serikali,” alisisitiza.

Akizungumzia kupanga kwa gharama za maisha alisema wabunge wa CCM wataipitisha bajeti hiyo huku kukiwa hakuna nyongeza yoyote ya mshahara.

“Kodi imeongezwa katika mafuta na itaathiri maisha ya wananchi wa kipato cha chini maana kipato chao kipo palepale. Pia kodi katika vinywaji, sigara na mafuta zitapanda na kuhatarisha kupanda kwa gharama za maisha kwa wananchi,” alisema.

Mbowe pia aligusia tofauti ya vitabu vya bajeti ya Serikali, kwamba kitabu cha mapato kinaonyesha kuwa Serikali kwa mwaka 2017/18 itakusanya Sh trilioni 23.9 wakati kitabu cha matumizi kinasema watatumia Sh trilioni 26.9 ikiwa ni ongezeko la Sh3 trilioni ambavyo vyanzo vyake havijaonyeshwa kwenye kitabu cha mapato

Upigaji kura

Akizungumzia upigaji wa kura ya ndio au hapana, Mbowe alisema tukio hilo ni kama muhuri tu kwa madai kuwa wanahalalishiwa kitu kilichokwisha hararishwa.

“Kwa utaratibu wa kupiga kura wa wazi wabunge wa CCM hawawezi kupiga kura ya hapana,” alisema Mbowe na kudai kuwa wabunge wa CCM walihongwa ili kuikubali bajeti hiyo jambo ambalo lilikanushwa na viongozi wa chama hicho tawala.

Ndio maana wabunge wa CCM waliishangilia sana bajeti hii wakati ikiwasilishwa bungeni. Pia nasikitishwa sana na mjadala wa bajeti kumezwa na ripoti za mchanga wa dhahabu. Watanzania wameshindwa kujua kasoro za bajeti hii,” alisema Mbowe.

Alifafanua: “Bajeti hii kwanza vitabu havilingani, vyanzo vya mapato si vya uhakika, vipaumbele si sahihi na inakwenda kuwakamua zaidi wananchi masikini.”

Alisema kwa kuwa wabunge wa upinzani ni wachache ndani ya chombo hicho cha dola hawana la kufanya zaidi ya kuwaachia wananchi kuhakikisha wanachagua wabunge wengi wa upinzani.

Ends
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo