Wasiolipa kodi ya majengo kushitakiwa


Nteghenjwa Hoseah, Arusha

WADAIWA sugu wa kodi ya majengo jijini hapa, watafikishwa mahakamani mwanzoni mwa Julai wakiendelea kukaidi kulipa kodi hiyo mwisho wa mwaka wa fedha wa 2016/17 unaomalizika Juni 30.

Mkuu wa Mkoa, Mrisho Gambo alitoa onyo hilo kwenye mkutano na waandishi wa habari kukumbusha wananchi kuhusu umuhimu wa kulipa kodi hiyo mapema kabla ya hatua kali kuchukuliwa dhidi ya wasiolipa.  

Alisema wamiliki wote wa majengo wanatakiwa kulipa kodi hiyo kwa mujibu wa sharia, lakini hali hairidhishi kwani wengi wao hawajajitokeza kulipa wakati Serikali inategemea fedha hizo kutekeleza miradi ya maendeleo.

Aliongeza kuwa muda uliowekwa wa malipo hayo unaelekea ukingoni ambapo Juni 30 ni mwisho na baada ya hapo, sheria kali zitachukuliwa kwa watakaobainika kuiibia Serikali kwa kutolipa mapato ya majengo wanayomiliki.

“Haiwezekani unamiliki nyumba halafu hutaki kuchangia kodi, ninatoa rai   wote kulipa kwa hiari, kwa sababu baada ya hapo ni faini ambayo ni mara tano ya kiasi ambacho ungetakiwa kulipa sasa au kupelekwa mahakamani kwa mujibu wa sheria.

Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wa Mkoa, Apili Mbarouk alisema hadi mwishoni mwa Mei walishakusanya Sh bilioni moja na siku zilizobaki wanatarajia kukusanya zaidi ya kiwango hicho.

Pia aliongeza kuwa katika maeneo ambayo hayajapimwa na kufanyiwa uthamini, wamiliki watalipa Sh 15,000 kwa mwaka na kwa maeneo ambayo yamefanyiwa uthamini wamiliki watalipa kwa kadri ya thamani ya jengo.

Aidha, aliwataka wafanyabiashara na wananchi kulipa na kudai risiti kwa kila biashara inayofanyika, ili kuhakikisha mapato ya Serikali yanakuwa salama na hayapotei.

“Katika hili, tutaanza ukaguzi katika maeneo yote ya mji huu kuanzia kwa wafanyabiashara na kuhakikisha wanatoa stakabadhi kwa wateja na ambaye atabainika hajatoa atapigwa faini ya Sh miloini 3 na kwa mwananchi ambaye atakuwa amenunua bidhaa bila kudai stakabadhi, atatozwa faini ya Sh 30,000.

Kikao hiki ni mwendelezo ya vikao maalumu vya kazi anavyofanya Mkuu wa Mkoa pamoja na TRA Mkoa, kuhakikisha mapato ya Serikali yanakusanywa kwa ufanisi ili kufikia malengo waliyojiwekea.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo