Leonce Zimbandu
Dk. Hamisi Kigwangala |
WAKAZI wa Mtaa wa Zogoali, Ilala
wamelalamikia Serikali kutelekeza zahanati yao kwa miaka mitatu sasa licha ya
naibu mawaziri wawili kuitembelea.
Mawaziri waliotembelea zahanati hiyo ni
Naibu Waziri wa Tamisemi, Seleman Jafo na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto, Dk Hamisi Kigwangalla
wakikagua zahanati 54 za Dar es Salaam ambazo hazijakamilika.
Mwenyekiti wa Mtaa huo, Swalehe Kiloko alisema
hayo alipozungumza na mwandishi wa habari hizi alipotembelea zahanati hiyo jana
kujua sababu za kutelekezwa zahanati hiyo.
Alisema ilianza kujengwa mwanzoni mwa mwaka juzi
hadi Septemba mwaka hui, ilifikia hatua ya kupauliwa lakini ilikwama hadi leo.
“Wananchi walifarijika baada ya mawaziri hao
kukagua jengo hilo na kuwapa matumaini, lakini ni miezi sita imepita sasa hakuna
kilichofanyika, hivyo sielewi sababu,” alisema.
Alisema anajua kuwa mawaziri hao walifanya
ziara hiyo lakini hajui kama zahanati zingine zimekamilika, ingawa bado
anaendeleza kilio chake hicho.
Aliongeza kuwa viongozi wa Manispaa
walipoulizwa na Naibu Waziri Jafo kuhusu mabati, walijibu kuwa yapo hiyo
kilichohitajika ni kupaua jengo hilo na si suala la bajeti.
Mkazi wa mtaa huo, Amina Said alisema kitendo
cha Serikali kuchelewa kukamilisha zahanati hiyo, kinafanya wajawazito
kujifungulia nyumbani kutokana na miundombinu mibovu.
Alisema kutokana na ubovu wa barabara, usafiri
unaotumika ni pikipiki kwa gharama ya Sh 4,000 hadi Sh 5,000 kwenda zahanati ya
Chanika.
“Watu wenye kipato cha chini hawawezi kumudu
gharama hizo, hivyo huchukua uamuzi wa kujifungulia nyumbani huku wakiomba Mungu,”
alisema.
Alisema zahanati hiyo ikikamilika, itasaidia
wananchi wa mitaa jirani, ikiwamo mitaa ya Homboza, Kimwani na Nzasa.
Msemaji wa Manispaa hiyo, Tabu Shaibu alisema
hawezi kutoa jibu lolote kuhusu ujenzi wa zahanati kwa vile yupo kwenye kikao.
“Nipo kwenye kikao siwezi kujibu lolote sasa,”
alisema.
0 comments:
Post a Comment