Venance Matinya, Mbeya
Jiji la Mbeya |
SIKU chache baada ya Chama cha Wakulima Tanzania (TASO)
kufutiwa usajili na kuzuiwa kujihusisha na makusanyo ya fedha kwa maandalizi ya
Maonesho ya Wakulima (Nanenane) mwaka huu, Serikali imejipanga kukusanya zaidi
ya Sh milioni 300 kupitia vyanzo vyake.
Akitoa juzi taarifa ya maandalizi ya maonesho na sherehe
za Nanenane mwaka huu Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, kwa niaba ya Sekretarieti
ya Kanda, Katibu Tawala Msaidizi wa Uchumi na Uzalishaji wa Mkoa, Nyasebwa Chimagu
alisema matarajio ni kukusanya Sh 335,543,801.
Alisema makusanyo hayo yanatarajiwa kutokana na vyanzo
mbalimbali vikiwamo vya ofisi za mkoa, halmashauri, tozo na ada za ushiriki
kutoka mashirika na taasisi za umma na binafsi.
Aliongeza kuwa kati ya hizo, Sh 138,443,801 zitatoka sekretarieti
za mikoa na halmashauri, huku Sh 197,100,000 zikitokana na vyanzo vingine kama
ada za ushiriki, tozo za viwanja, viingilio na ushuru uwanjani.
Chimagu alisema hali ya makusanyo hadi Julai 6
hairidhishi, kwani ni Sh milioni 35 tu zilizokusanywa kutoka baadhi ya
sekretarieti za mikoa na Halmashauri.
Kwa hali hiyo, Mwenyekiti wa Kikao hicho ambaye pia ni
Mkuu wa Mkoa, Amos Makalla aliagiza halmashauri na mikoa yote kuhakikisha
inamaliza kutoa michango yao hadi Julai 15.
Alisema ili kukamilisha maandalizi ya maonesho, kinachotakiwa
ni fedha hivyo ni vema halmashauri zikajipanga mapema kuruhusu sekretarieti
kuandaa sherehe vizuri.
Wakuu wa Mikoa ya Njombe na Ruvuma, Christopher ole
Sendeka na Dk Binilith Mahenge walisisitiza washiriki kutoa michango yao mapema
ili kufanya maandalizi mapema ikiwa ni pamoja na kujiandaa na maonesho ya
kimataifa.
Walisema endapo hadi Julai 15 kutakuwa na halmashauri isiyomaliza
madeni yake, itazuiwa kushiriki maonesho ya Nanenane mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment