Mwandishi Wetu
Reli |
SERIKALI imetoa miezi sita kwa wakazi wa
Mpanda mkoani Katavi kuondoka maeneo ya hifadhi za reli ili kupisha maboresho
yanayoendelea kufanywa na Shirika la Reli Tanzania (TRL) kwenye miundombinu
yake.
Agizo hilo la Serikali lilitolewa juzi na
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngoyani akizungumza na wafanyakazi
wa taasisi zilizo chini ya wizara yake mkoani Katavi ambapo alisema ni wakati
sasa kwa wananchi kufuata sheria kwa kutovamia miundombinu hiyo.
“Ninatoa miezi sita kuanzia sasa,
itakapofika Januari mwakani wananchi wote watakaokuwa ndani ya hifadhi ya reli
watabomolewa nyumba kwa kuzingatia sheria zinazolinda miundombinu,” alisema
Ngonyani.
Aidha, Ngonyani aliuagiza uongozi wa mkoa
kusimamia wananchi kuhama na kuhakikisha kila aliyevamia miundombinu anabomoa
nyumba yake kabla ya sheria kufuata mkondo wake.
Naibu Waziri aliwahadharisha wafanyakazi
wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuzingatia maslahi ya Taifa wakati wa
kutafuta zabuni.
Ngonyani pia alikagua barabara ya
Kanazi-Kizi-Kibaoni (Km 76.6), Sumbawanga-Kanazi (Km 75) na kuiagiza TANROADS mkoa
wa Rukwa kuweka mizani kwenye barabara zinazojengwa, ili kudhibiti magari
makubwa yanayozidisha uzito na kusababisha
uharibifu kwa barabara za mkoa huo.
“Ni wakati sasa wanaotoa huduma za
usafirishaji mizigo kufuata sheria na
kubeba mzigo wa uzito stahiki, kwa sababu madereva hao hao wakienda nchi jirani
wanafuata sheria kwa umakini, SUMATRA simamieni utoaji wa leseni kwa magari ya
abiria na mizigo kwa kuzingatia uzito wa magari ili kuziweshesha barabara zetu
zidumu,” alisema Ngonyani.
Meneja wa TANROADS wa Mkoa wa Rukwa, Msuka
Mkina alimhakikishia Ngonyani kwamba wakala wake utahakikisha mizani
inawekwa sehemu za barabara ili kubaini magari yanayozidisha uzito na
kuyachukulia hatua za kisheria.
Ngonyani anafanya ziara ya kukagua
miundombinu ya barabara, viwanja vya ndege, ujenzi wa nyumba za viongozi, huduma
za mawasiliano ya simu na madaraja
katika mikoa ya Katavi na Rukwa.
0 comments:
Post a Comment