Suleiman Msuya
Mamlaka ya Mapato Tanzania |
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA)
imekusanya Sh trilioni 14.4 kwa mwaka wa fedha 2016/17.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Huduma
na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo na kubainisha kuwa makusanyo
hayo ni sawa na ongezeko la asilimia 7.67 ikilinganishwa na ya mwaka 2015/16 ambayo
yalikuwa Sh trilioni 13.3.
Taarifa ya mwaka ya TRA inatoka huku
ikiwa haijaainisha makusanyo ya kila mwezi na kuwa kiasi hicho cha mwaka kikigawanywa
kinaonesha kuwa kwa kila mwezi Mamlaka hiyo ilikusanya Sh trilioni 1.2.
Kayombo alisema sambamba na makusanyo, TRA
imeendelea kukusanya kodi ikiwamo ya majengo ambapo mwitikio wake ni wa kiwango
cha kuridhisha.
“Mamlaka inapenda kuwashukuru walipakodi
wote kwa mwitikio huo na wengine wanaoendelea kujitokeza kwenye ofisi
mbalimbali za Mamlaka nchi nzima, ili kulipa kodi hiyo ambayo mwisho ni Julai
15.
Aidha, alisema TRA inatoa mwito kwa
wafanyabiashara kutoa risiti za mashine za elektroniki - EFDs pindi wanapouza
bidhaa au kutoa huduma na wananchi wahakikishe wanazidai wanaponunua bidhaa au
kupata huduma na kinyume chake watakuwa wanatenda kosa kwa mujibu wa sheria ya
usimamizi wa kodi.
Mkurugenzi huyo alisema hivi sasa TRA
inaendelea na mchakato wa uhamasishaji na ukaguzi sehemu zote za biashara dhidi
ya wafanyabiashara wasiotumia EFDs na kuhimiza wananchi kudai risiti wanunuapo
bidhaa au kupata huduma.
“Napenda kuwakumbusha wananchi wote
kuhakiki risiti zao, ili kuona usahihi wa tarehe na kiasi walicholipa kabla ya
kuondoka,” alisistiza Kayombo.
0 comments:
Post a Comment