Suleiman Msuya
Dk.John Magufuli |
RAIS John Magufuli amemteua Profesa
Florens Luoga kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA).
Profesa Luoga anachukua nafasi ya
Bernard Mchomvu ambaye Bodi yake ilivunjwa na uteuzi wake kutenguliwa Novemba
20 mwaka jana na Rais Magufuli.
Luoga ameteuliwa kushika nafasi hiyo
akitokea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ambako ni Naibu Makamu Mkuu wa
Chuo hicho Taaluma.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, uteuzi
wa Profesa Luoga ulianza jana.
Uvunjwaji wa Bodi ya awali ulitangazwa
na Rais Magufuli wakati akiongoza Mahafali ya 31 ya Chuo Kikuu Huria
yaliyofanyika Kibaha, Pwani ambako alisema Bodi hiyo iliidhinisha Sh bilioni 6
zilizotengwa kwa matumizi ya TRA kupelekwa kwenye benki kwenye akaunti ya muda
maalumu.
“Bodi imepitisha fedha kwenda kwenye
akaunti ya muda maalumu kinyume na maagizo ya Serikali, ndiyo maana
nilipozipata hizo fedha nimezichukua na Bodi kwa heri,” alisema.
“Kumekuwa na mchezo huu kwa wakurugenzi
watendaji wengi zinapotolewa fedha kwa ajili
ya kwenda kwenye miradi fulani, zile fedha wanazochukua wanaziweka kwenye benki
za biashara, na kuweka akaunti maalumu kwa mazungumzo ya uelewano kati ya huyo
mkuu wa taasisi na benki husika. Waziri hiyo message sent and delivered,”
alisisitiza.
Wasifu
Profesa Luoga alizaliwa mwaka 1958 na
mwaka 1985 alipata Shahada ya Kwanza ya Sheria katika Chuo Kikuu cha UDSM,
mwaka 1988 alihitimu Shahada ya Pili ya Uzamili ya Chuo Kikuu cha Queen’s cha
Canada na mwaka 1991 alihitimu Shahada ya Uzamili katika Sheria za Kimataifa
kwenye Chuo cha Lund, Sweden.
Mwaka 2003 alitunukiwa Shahada ya
Uzamivu kwenye Chuo Kikuu cha Warwick cha Uingereza.
Aidha, mwaka 1986, Profesa Luoga
aliajiriwa UDSM katika Kitivo cha Sheria kama Mhadhiri Msaidizi ambapo mwaka
2005 alipandishwa kuwa profesa.
Pia alishika nafasi mbalimbali za
utawala chuoni hapo kama Mwenyekiti Kamati ya Msaada wa Kisheria katika Kitivo
cha Sheria kuanzia mwaka 1993 hadi 1995.
Profesa Luoga alipandishwa kuwa Mkuu wa
Utawala Kitivo cha Sheria mwaka 1992 hadi 1995, Mkurugenzi wa Shahada ya Kwanza
mwaka 2005 hadi 2009, Kaimu Naibu Mkuu wa Chuo Taaluma mwaka 2013 hadi sasa na
pia ni Wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Hali kadhalika Profesa Luoga ametoa
machapisho mbalimbali kuhusu kodi, haki za binadamu, sheria na manunuzi.
0 comments:
Post a Comment