Mwandishi Wetu, Lindi
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa |
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amekagua ujenzi wa daraja la
Mto Lukuledi lenye urefu wa kilometa 30.45 likiunganisha mikoa ya Lindi na
Mtwara na kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi huo.
Amesema ujenzi wa daraja hilo unatakaogharimu Sh bilioni
5.4 ni mkombozi kwa wananchi wa mikoa hiyo hasa wilaya za Ruangwa na Masasi,
ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakishirikiana katika masuala ya kilimo na
kijamii.
Waziri Mkuu alisema hayo jana kwenye daraja hilo katika
kijiji cha Nandanga alipowasili Ruangwa akiwa katika siku ya pili ya ziara yake
ya kikazi ya siku nne mkoani Lindi.
“Watu wengi wamepoteza maisha kwa kuliwa na mamba
wakikatiza eneo hili. Ujenzi wa daraja hili ni muhimu, watu wengi wa Ruangwa
wanavuka kufuata matibabu hospitali ya Ndanda, Masasi na wa Ndanda wanavuka
kufanya shughuli za kilimo Ruangwa,” alisema Majaliwa.
Waziri Mkuu aliomba wananchi wa maeneo hayo kuhakikisha
wanatoa ushirikiano kwa mkandarasi anayejenga daraja hilo, ili aweze kutekeleza
majukumu yake ipasavyo na kumaliza mradi huo kwa wakati.
Mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe aliipongeza Serikali kwa
jitihada zake za kuwaletea wananchi maendeleo na kubadilisha maisha yao.
Alisema mradi wa daraja hilo ni faraja kwa wananchi wa
mikoa hiyo kwa kuwa eneo hilo ni makazi ya mamba, hivyo kukamilika kwake
kutaokoa maisha ya watu na kurahisisha usafiri wa watu na bidhaa.
Waziri Mkuu pia alisema changamoto ya upatikanaji huduma
ya maji safi na salama katika vijiji vya Litama, Luchelegwa, Nandanga, Ipingo
na Chiapi itakuwa historia baada ya kuunganishwa mradi wa maji wa
Mbwinji.
Alisema hayo alipozungumza kwa nyakati tofauti na
wananchi wa Litama, Chiapi, Nandanga, Luchelegwa alipowasili Ruangwa.
Majaliwa alisema Serikali inatekeleza kampeni yake
ya kumtua mama ndoo, hivyo itahakikisha wananchi, hususan vijijini,
wanapata huduma ya maji safi na salama umbali usiozidi meta 400.
Waziri Mkuu pia alizindua zahanati ya Nandanga ambayo
imejengwa kwa fedha za Mfuko wa Jimbo kwa Sh milioni 73.47 na kuwahakikishia
kwamba Serikali itawapelekea wataalamu wa kutosha kuwahudumia.
0 comments:
Post a Comment