Grace Gurisha
RAIA wa Uganda, Edwin Gusongoirye (30) na mfanyabiashara,
Steven Simon (45) wamefikishwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,
wakikabiliwa na tuhuma za uhujumu uchumi kwa kuisababishia Serikali hasara ya
Sh milioni 210.2.
Gusongoirye ambaye pia ni mfamasia na Simon walifikishwa
mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi, Godfrey
Mwambapa.
Akisoma mashitaka hayo, Wakili Mwandamizi wa Serikali,
Nassoro Katuga alidai kuwa kati ya Machi 6 na Juni 22, Dar es Salaam,
washitakiwa walitengeneza mfumo wa kutumia huduma za mtandao kukwepa kodi ya
kupokea na kusambaza mawasiliano bila kibali.
Pia kati ya Machi 6 na Juni 22, mwaka jana washitakiwa
hao waliendesha mfumo wa kupokea na kusambaza mawasiliano ya kimataifa bila leseni
ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Katuga alidai katika mashitaka ya tatu kuwa katika tarehe
na mwaka huo huo, Gusongoirye na Simon waliingiza vifaa vya mawasiliano nchini
ambavyo ni makasha matatu ya simu bila kibali cha TCRA.
Katika mashitaka ya nne, ilidaiwa kuwa kabla ya Machi,
2012 washitakiwa walisimika vifaa vya mawasiliano zikiwamo kompyuta mpakato
mbili aina ya Dell na Hp bila kibali.
Pia ilidaiwa kuwa washitakiwa walitumia vifaa vya mawasiliano
ambavyo havijathibitishwa kwa lengo la kupokea na kusambaza viashiria vya
mawasiliano bila kuthibitishwa na TCRA.
Katuga alidai pia kuwa Machi 6 na Juni 22, kwa makusudi
na kwa pamoja waliisababishia Serikali hasara ya Sh milioni 210.2.
Washitakiwa hawakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa Mahakama
hiyo haina mamlaka ya kusikiliza mashitaka ya uhujumu uchumi na kwamba haiwezi
kutoa dhamana, kwani mashitaka hayo ni ya zaidi ya Sh milioni 10 ambayo
wanatakiwa kuomba Mahakama Kuu.
Katuga alidai kuwa upelelezi wa shauri hilo haujakamilika
na kuomba tarehe nyingine ya kesi kutajwa na Hakimu Mwambapa aliiahirisha hadi
Julai 25, itakapotajwa.
0 comments:
Post a Comment