Suleiman Msuya
Daraja la Kigamboni |
WAKAZI wa Wilaya ya Kigamboni, wataanza
kulipia Sh. 3,000 kwa mwezi kwa ajili ya uchangiaji uzoaji taka ikiwa ni
mikakati ya wilaya hiyo kuwa na mazingira safi.
Hayo yamesemwa na mkuu wa wilaya hiyo, Hashimu
Mgandilwa wakati akizindua mpango wa uchangiaji uzoaji taka kila kaya huku
akibainisha kuwa kiasi hicho ni sawa na kutoa sh. 100 kila siku kwa kaya.
Mgandilwa alisema mpango huo utasaidia
kupunguza suala la uchafu katika wilaya hiyo na gharama zake ni nafuu tofauti
na awali ambapo kaya moja kwa kata ya Kibada walilazimika kulipa kiasi cha Sh. 20000
mpaka 40,000 jambo ambalo ni changamoto kwa wakazi hao.
Alisema Serikali ya Awamu ya Tano chini
ya Rais John Magufuli imedhamiria kurahisisha maisha kwa wananchi wake, hivyo
ni imani yake kuwa kila mwananchi ataweza kuchangia kiasi hicho cha sh. 3,000.
“Mradi huo utasaidia changamoto
iliyojitokeza ya baadhi ya watu kutupa taka kwenye fukwe ya bahari, lakini pia
utaratibu huu utasaidia kukabiliana na magonjwa ambayo yanazulika,” alisema.
Aidha, mkuu huyo wa wilaya amewaomba
wananchi katika kaya mbalimbali kutunza taka zinazozalishwa majumbani mpaka
magari ya mradi yatakapokuja kuzichukua zikiwa katika mazingira mazuri.
Alisema tafiti zinaonesha kuwa chanzo kikubwa
cha magonjwa ya milipuko kinatokana na kuzagaa kwa takataka kwenye mazi ya watu
hivyo ni jukumu la kila mwananchi kuhakikisha anakuwa mlinzi kwa mwenzake
kuhusu utupaji taka.
Mgandilwa alisema mkakati wa halmashauri
ni kuhakikisha mradi huo unakuwa wa uhakika na kuwa magari nane ambayo
yamepatikana kwa sasa yatazunguka kata zote.
“Halmashauri haina uwezo wa kutoa
msisitizo kila wakati ili watu watunze mazingira hivyo ni jukumu la Wanakigamboni
kutunza mazingira kwa faida yetu,” alisema.
Alisema utaratibu huo utawahusu hadi
wamiliki wa hoteli na taasisi mbalimbali ambao wao wamewekewa kiasi ambacho ni
nafuu kwao.
Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Steven
Katemba ameeleza kuwa mradi huo utawanufaisha vijana zaidi ya 134 na utaanza
kwa kata tano ikiwemo Kigamboni, Mjimwema, Tungi, Kibada na Vijibweni.
Alisema mipango ya halmashauri ni
kukamilisha ujenzi wa dampo la Lingato ambapo bilioni moja imetengwa na halmashauri
ya Jiji kwa ajili ya ukarabati wa dampo hivyo ndani ya miezi kadhaa ukarabati
utakwisha na taka hazitakuwa zinapelekwa huko.
0 comments:
Post a Comment