Wanaume 27,000 kutahiriwa mwaka huu


Venance Matinya, Mbeya

ILI kupunguza maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi na magonjwa ya njia ya mkojo mkoani Songwe, zaidi ya wanaume 26,556 wanatarajiwa kufanyiwa tohara kwa mwaka huu.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni ya kuhamasisha tohara kwa wanaume mkoani humo kwenye viwanja vya shule ya msingi ya Tunduma, Mshauri wa Ufundi wa Tohara (WRP) wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Dk Zegeli Balishanga alisema wizara kwa kushirikiana na wadau HJFMRI imeandaa kampeni ya siku 28 ili kufikia malengo ya kutahiri wanaume hao.

Alisema imebainika kuwa Songwe na Mbeya iko kwenye kiwango kikubwa cha maambukizi ya Ukimwi kwa asilimia tisa kutokana na wanaume wengi kutotahiriwa, hivyo kuambukizwa kirahisi na kuambukiza wenzao.

Aliongeza kuwa tohara inasaidia kumkinga mwanamume dhidi ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi kwa asilimia 60 hivyo itasaidia kupunguza idadi ya waathirika wa Ukimwi na kupunguza uwezekano wa kupata magonjwa ya zinaa, kukinga saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake na saratani ya uume.

Alizitaja faida zingine kuwa ni kupunguza magonjwa ya njia ya mkojo kwa wanaume, kurahisisha usafi na kumfanya mwanamume kujiamini zaidi kuliko kuishi bila tohara, hususani akiwa na umri mkubwa.

Innocent Ndunguru, Mratibu wa WRP wa Mkoa wa Songwe, alisema ili kufikia malengo, mkoa umetenga vituo vinane vya tohara ambavyo ni hospitali ya Misheni ya Mbozi, zahanati za Nyimbili, Namabinzo, Ihanda, Myunga, Mkulwe, Chitete na Magamba.

Alisema kampeni hiyo yenye kaulimbiu ya ‘Amka sasa, Wahi tohara, kuwa msafi, pata kinga’, inalenga jamii kupata ujumbe ili kufahamu umuhimu wa tohara katika kupambana na maambukizi.

Aliongeza kuwa kampeni hiyo inalenga kutahiri wanaume 13,911 sawa na asilimia 52 ya malengo yaliyotolewa na Serikali kwa mwaka kwa Songwe ambako kuna mwitikio mkubwa uliofanya wanaume 11,286 sawa na asilimia 81 kutahiriwa ndani ya muda wa kampeni.

Nao watoa huduma za tohara, Neema Mahenge na Wilson Kasanga walisema wanaume wengi walijitokeza huku wengine wakisindikizwa na wenza wao.

“Wengi wanakuja na watoto na wajukuu zao na hutahiriwa kwa pamoja bila woga na wachache wanasindikizwa na wenza wao, ambao wako kwenye uhusiano wakitarajia kufunga ndoa jambo linaloashiria elimu kuwafikia vizuri,” alisema Kasanga.

Waliongeza kuwa changamoto kubwa wanayokabiliana nayo ni imani potofu kwa baadhi ya jamii ambazo zimekuwa zikidai kuwa ngozi iliyokatwa baada ya tohara hutaka waizike jirani na nyumbani kwao jambo linalowasababishia usumbufu.

Awali mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa kampeni hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Momba, Juma Irando kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Chiku Galawa alitoa mwito kwa jamii na wananchi kujitokeza kwa wingi kufanyiwa tohara bure.

Aidha, alitoa mwito kwa watoa huduma kuongeza kasi na ufanisi wa kazi hiyo ili kuendana na mwitikio mzuri wa wananchi waliokubali kufanyiwa tohara kwa hiari yao.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo