Masamaki wa TRA, wenzake wako huru

Tiagi Masamaki
*Mkurugenzi Mashitaka apoteza nia kuendelea kuwashitaki
*Wengine watatu waachwa, wasomewa mashitaka mapya 110

Grace Gurisha


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imemwacha huru aliyekuwa Kamishna wa Forodha na Ushuru wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Tiagi Masamaki na wenzake.

Walioachwa walikuwa wakikabiliwa na mashitaka ya uhujumu uchumi na kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 12.7.

Watuhumiwa hao waliachwa huru jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi baada ya Wakili wa Serikali Mkuu, Timon Vitalis kuiomba Mahakama iwaache chini ya kifungu cha 91(1) cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).

Hiyo imetokana na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kukosa nia ya kuendeleza mashitaka dhidi yao na Hakimu Shaidi kukubali.

Mbali na Masamaki, wengine walioachwa ni waliokuwa Meneja Kitengo cha Huduma za Ushuru wa TRA, Habib Mponezya, Meneja Msimamizi na Ufuatiliaji wa Forodha, Burton  Mponezya na Msimamizi Mkuu Kitengo cha Ushuru wa Forodha (ICD) Azam, Eliachi  Mrema na Meneja wa Azam ICD, Ashrafu Khan.

Hata hivyo,  baada ya kesi hiyo kufutwa na washitakiwa hao kuachwa huru, wenzao ambao ni waliokuwa Mchambuzi Mwandamizi  wa Masuala ya Biashara  wa TRA,  Hamis Omary, Meneja wa Oparesheni  za Usalama na Ulinzi wa ICD, Raymond Louis na Haroun Mpande wa Kitengo cha Mawasiliano ya Kompyuta ICT TRA walisomewa  mashitaka mapya 110 na wenzao wawili.

Katika mashitaka hayo ya uhujumu uchumi yamo ya kufuta data kwenye mfumo wa kompyuta, kughushi na kutakatisha fedha.

Masamaki na wenzake walikuwa wanadaiwa kuwa kati ya Juni mosi na  Novemba 17 mwaka juzi, walikula njama na kuidanganya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu Sh bilioni 12.7.

Historia

Masamaki na wenzake walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Desemba mwaka juzi ikiwa ni kesi ya kwanza ya madai ya rushwa kufikishwa mahakamani tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani.

Katika kesi hiyo, kwa mara ya kwanza watu wanane kati ya 12 waliokuwa wakishikiliwa na kuhojiwa na Polisi kwa kashfa ya upotevu wa kontena 329 na ukwepaji ushuru wa zaidi ya Sh billion 80 walifikishwa kortini Desemba 4, 2015.

Watuhumiwa hao walikuwa wakikabiliwa na mashitaka mawili likiwamo la kuhujumu uchumi na upotevu wa Sh billion 12.7 na kuisababishia hasara Serikali.

Ilidaiwa mahakamani hapo, kwamba Masamaki na wenzake, walikula njama kutoa kontena kwenye bandari ya Dar es Salaam na kuzipeleka bandari kavu, huku wakidai kuwa kontena hizo zilishalipiwa kodi.

Kwenye mashitaka ya uhujumu uchumi, Masamaki na wenzaki walikuwa wakituhumiwa kuisababishia hasara ya mabilioni ya fedha Serikali, ambazo ni mapato na kodi, mashitaka ambayo hayakustahili dhamana kwa kuwa Mahakama ya Kisutu haina uwezo wa kisheria kusikiliza shauri hilo.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo