Kairuki akanusha taarifa potofu za mafao


Hussein Ndubikile

Angella Kairuki
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki amesema Serikali haijatoa tamko kuhusu hatima ya mafao ya watumishi wa umma waliokutwa na vyeti bandia, huku akibainisha kuwa tamko litatolewa baada ya uhakiki wa vyeti hivyo kukamilika.

Kauli hiyo aliitoa jana Dar es Salaam wakati akizungumza na watumishi wa Manispaa ya Kinondoni.

Alisema kuna taarifa za upotoshaji kwenye mitandao zikieleza kwa namna tofauti jambo hilo hali inayosababisha sintofahamu miongoni mwa wahusika na kusisitiza kuwa ufafanuzi utatolewa uhakiki utakapokamilika.

"Hakuna tulikosema watalipwa au hawatalipwa mafao yao, mwisho wa uhakiki Serikali itatoa ufafanuzi," alisema Kairuki.

Waziri Kairuki aliwataka watumishi wa manispaa kuacha kusambaza taarifa za Serikali, kwani kufanya hivyo ni kwenda kinyume na Sheria ya Makosa ya Mtandao ya Mwaka 2015.

Aliongeza kuwa changamoto zinazoikabili Manispaa ya Kinondoni zitafafutiwa ufumbuzi zikiwamo za upungufu wa walimu 50 wa shule za msingi, watumishi 371 wa afya na watumishi wa ardhi na mipango.

Aliwakumbisha maofisa utumishi wa Manispaa kuwafanyia uhakiki watumishi kabla hawajaingizwa kwenye mfumo malipo ya mishahara na kwamba Serikali kwenye bajeti ya mwaka 2017/18 kuanzia mwezi huu hadi Septemba itatoa vibali 52,476 vya ajira mpya.

Alishauri watumishi hao kujikinga na Ukimwi kwa kubadili nyendo zao na kushiriki kufanya ili kujiepusha na magonjwa yasiyoambukiza.

Ofisa Utumishi Mkuu wa Manispaa hiyo, Anna Mwakalyelye alisema hadi sasa mashauri ya nidhamu 134 yanashughulikiwa, 48 yameshashughulikiwa huku 80 yakiendelea kufanyiwa kazi.

Alisema Manispaa imetenga fedha za kujenga na kuzifanyia ukarabati ofisi za kata za Kinondoni.

Alifafanua kuwa watumishi 372 walipandishwa vyeo na tisa kufanyiwa mabadiliko ya vyeo kulingana na vigezo vyao.

Pia alisema watumishi wanaendelea kupata mafunzo ili kuwasaidia kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Mkuu wa Wilaya, Ali Hapi alimpongeza Waziri Kairuki kwa utendaji kazi wake na kumwomba atazame kero za upungufu wa watumishi.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo