Panga pangua Uwanja wa Kimataifa wa JK Nyerere


Mwandishi Wetu

SERIKALI imeagiza uongozi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), kupitia upya mikataba minne ya watoa huduma kwenye uwanja huo, kutokana na kugubikwa na utata huku ikisisitiza kubadilisha uongozi huo.

Pia imesisitiza kuwa wiki ijayo itaunda timu ya wataalamu wa kupitia mikataba hiyo minne, pamoja na mingine inayohusu uwanja huo lengo likiwa kuiboresha ili ilete tija.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, alisema hayo jana wakati alipotembelea uwanja huo kufanya ukaguzi katika maeneo mbalimbali.

Profesa Mbarawa alisema kwa kiasi kikubwa mikataba iliyopo imegubikwa na utata na kwamba ipo inayoonesha kuwa watoa huduma huo wanalipa kwa mwezi, tofauti na makubaliano kuwa malipo yafanyike kila mwaka.

“Hapa inaonekana watoa huduma wanalipa kila mwezi, wakati makubaliano ni kila mwaka jambo ambalo ni changamoto, hivyo iangaliwe ili tuibadilishe. Wiki ijayo nitaunda timu ya wataalamu kwa ajili ya kupitia mikataba hiyo minne na mingine yote inayohusu uwanja huu,”alisema.

Alisema waliotayarisha mikataba hiyo kwa kiasi kikubwa hawakuangalia itanufaisha vipi Taifa, hivyo kupitiwa upya kutasaidia Serikali na wafanyabaishara kupata wanachostahili.

Aliongeza kuwa tangu awali mikataba hiyo haikuwa mizuri kwa kuwa hakuna kodi zilizokuwa zikikusanywa, hali iliyoikosesha Serikali mapato.

Kuhusu uongozi, Profesa Mbarawa alisema ipo haja ya kufanyika maboresho ya uongozi wa uwanja huo na vingine, ili usimamie vizuri viwanja hivyo kwa kukusanya kodi kwa mujibu wa sheria badala ya kusuasua.

“Kama viwanja vya ndege nchini vikisimamiwa vizuri, vina uwezo wa kukusanya kodi nyingi na maeneo ambayo awali yalikuwa hayakusanywi kodi, na sasa zinakusanywa yanaonesha mafanikio makubwa,”alisema.

Alisema kwa kiasi kikubwa uongozi uliopo sasa ni mzuri, lakini hauendani na kasi anayotaka hivyo kunatakiwa kuwepo watoahuduma ambao watakuwa wazalendo wa kukusanya kodi.

“Hata kama mtu una matatizo, lazima uwe mbunifu ili yaishe lakini si kusema kila siku kwamba ni ya kawaida wakati ukiyaacha yanaendelea kukua jambo ambalo halifai kwa kiongozi,”alisema.

Aliutaka uongozi wa uwanja huo, Idara ya Uhamiaji na Benki ya NMB kuhakikisha wanakaa pamoja kuangalia namna ya kutatua changamoto ya utoaji huduma katika eneo hilo, ili wageni wanapoingia nchini wasitumie muda mrefu.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Salim Msangi alifafanua kuwa licha ya kuwepo chagamoto nyingi kwenye eneo hilo, wamekuwa wakitafuta njia mbadala za kuzipunguza ili uwanja ulete tija.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo