Majaliwa aipongeza NHC kujenga zahanati


Mwandishi Wetu, Lindi 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ameupongeza uongozi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa kukamilisha ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Mnolela mkoani hapa kwa muda mfupi.

Amesema ujenzi wa zahanati hiyo ya kisasa ulianza Machi na sasa umekamilika, jambo ambalo litarahisisha upatikanaji huduma za afya kwa wananchi wa eneo hilo na jirani.

Waziri Mkuu alitoa pongezi hizo juzi alipozungumza na wananchi wa kijiji cha Mnolela baada ya kuzindua zahanati hiyo iliyosimamiwa na NHC.

Alisema ujenzi wa zahanati hiyo ni mwendelezo wa mkakati wa Serikali kuboresha huduma za afya kwa kuzisogeza karibu na wananchi.

“Rais John Magufuli amedhamiria kuondolea wananchi changamoto za huduma za afya, hivyo tuendelee kumwunga mkono,” alisema Waziri Mkuu.

Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu alisema mradi wa ujenzi wa zahanati hiyo ulisimamiwa na shirika lake kwa Sh milioni 65.5.

“Sh milioni 15 zilitolewa na Rais, Sh milioni 10 na Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye huku NHC ikitoa Sh milioni 10 na kiasi kilichosalia ni mchango wa Halmashauri,” alisema.

Awali Nape alimshukuru Rais Magufuli kwa mchango mkubwa alioutoa kwenye ujenzi wa zahanati hiyo.

Nape alisema zahanati hiyo ni mkombozi kwa wakazi wa kijiji cha Mnolela na wananchi wengine wanaoishi maeneo jirani.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo