Wananchi walalamika zahanati kutelekezwa


Leonce Zimbandu

Dk. Hamisi Kigwangala
WAKAZI wa Mtaa wa Zogoali, Ilala wamelalamikia Serikali kutelekeza zahanati yao kwa miaka mitatu sasa licha ya naibu mawaziri wawili kuitembelea.

Mawaziri waliotembelea zahanati hiyo ni Naibu Waziri wa Tamisemi, Seleman Jafo na Naibu Waziri wa  Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamisi Kigwangalla wakikagua zahanati 54 za Dar es Salaam ambazo hazijakamilika.

Mwenyekiti wa Mtaa huo, Swalehe Kiloko alisema hayo alipozungumza na mwandishi wa habari hizi alipotembelea zahanati hiyo jana kujua sababu za kutelekezwa zahanati hiyo.

Alisema ilianza kujengwa mwanzoni mwa mwaka juzi hadi Septemba mwaka hui, ilifikia hatua ya kupauliwa lakini ilikwama hadi leo.

“Wananchi walifarijika baada ya mawaziri hao kukagua jengo hilo na kuwapa matumaini, lakini ni miezi sita imepita sasa hakuna kilichofanyika, hivyo sielewi sababu,” alisema.

Alisema anajua kuwa mawaziri hao walifanya ziara hiyo lakini hajui kama zahanati zingine zimekamilika, ingawa bado anaendeleza kilio chake hicho.

Aliongeza kuwa viongozi wa Manispaa walipoulizwa na Naibu Waziri Jafo kuhusu mabati, walijibu kuwa yapo hiyo kilichohitajika ni kupaua jengo hilo na si suala la bajeti.

Mkazi wa mtaa huo, Amina Said alisema kitendo cha Serikali kuchelewa kukamilisha zahanati hiyo, kinafanya wajawazito kujifungulia nyumbani kutokana na miundombinu mibovu.

Alisema kutokana na ubovu wa barabara, usafiri unaotumika ni pikipiki kwa gharama ya Sh 4,000 hadi Sh 5,000 kwenda zahanati ya Chanika.

“Watu wenye kipato cha chini hawawezi kumudu gharama hizo, hivyo huchukua uamuzi wa kujifungulia nyumbani huku wakiomba Mungu,” alisema.

Alisema zahanati hiyo ikikamilika, itasaidia wananchi wa mitaa jirani, ikiwamo mitaa ya Homboza, Kimwani na Nzasa.

Msemaji wa Manispaa hiyo, Tabu Shaibu alisema hawezi kutoa jibu lolote kuhusu ujenzi wa zahanati kwa vile yupo kwenye kikao.

“Nipo kwenye kikao siwezi kujibu lolote sasa,” alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo