TRA yakusanya trilioni 14/-


Suleiman Msuya

Mamlaka ya Mapato Tanzania
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imekusanya Sh trilioni 14.4 kwa mwaka wa fedha 2016/17.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo na kubainisha kuwa makusanyo hayo ni sawa na ongezeko la asilimia 7.67 ikilinganishwa na ya mwaka 2015/16 ambayo yalikuwa Sh trilioni 13.3.

Taarifa ya mwaka ya TRA inatoka huku ikiwa haijaainisha makusanyo ya kila mwezi na kuwa kiasi hicho cha mwaka kikigawanywa kinaonesha kuwa kwa kila mwezi Mamlaka hiyo ilikusanya Sh trilioni 1.2.

Kayombo alisema sambamba na makusanyo, TRA imeendelea kukusanya kodi ikiwamo ya majengo ambapo mwitikio wake ni wa kiwango cha kuridhisha.

“Mamlaka inapenda kuwashukuru walipakodi wote kwa mwitikio huo na wengine wanaoendelea kujitokeza kwenye ofisi mbalimbali za Mamlaka nchi nzima, ili kulipa kodi hiyo ambayo mwisho ni Julai 15.

Aidha, alisema TRA inatoa mwito kwa wafanyabiashara kutoa risiti za mashine za elektroniki - EFDs pindi wanapouza bidhaa au kutoa huduma na wananchi wahakikishe wanazidai wanaponunua bidhaa au kupata huduma na kinyume chake watakuwa wanatenda kosa kwa mujibu wa sheria ya usimamizi wa kodi.

Mkurugenzi huyo alisema hivi sasa TRA inaendelea na mchakato wa uhamasishaji na ukaguzi sehemu zote za biashara dhidi ya wafanyabiashara wasiotumia EFDs na kuhimiza wananchi kudai risiti wanunuapo bidhaa au kupata huduma.

“Napenda kuwakumbusha wananchi wote kuhakiki risiti zao, ili kuona usahihi wa tarehe na kiasi walicholipa kabla ya kuondoka,” alisistiza Kayombo.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo