Majaliwa: Mgonjwa asikose dawa hospitalini


Mwandishi Wetu

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema hakuna mgonjwa atakayekwenda kutibiwa kwenye hospitali, vituo vya afya au zahanati akakosa dawa kwani Serikali imetenga fedha nyingi za  kununulia dawa na vifaa tiba.

Majaliwa alisema hayo juzi, akizungumza na wananchi wa wilaya ya Liwale kwenye mkutano wa hadhara.

Waziri Mkuu anayefuatana na mkewe, Mary katika ziara ya kikazi ya siku nne mkoani humo, alisema Serikali haitaki kusikia wananchi wakikosa dawa. 

Alisema moja kati ya ajenda muhimu za Serikali ni kuboresha huduma za afya kwa wananchi, ambapo kila mwezi halmashauri zote nchini zinapelekewa fedha za dawa. 

“Serikali ya Rais John Magufuli inatoa fedha za kununulia dawa kila mwezi katika halmashauri zote nchini. Sasa kama hapa Liwale kuna malalamiko ya wananchi kukosa dawa, Mkuu wa Wilaya kafuatilie huko Halmashauri ili kujua wanapeleka wapi fedha za dawa,” alisema. 

Katika Bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ya mwaka wa fedha 2017/18 Sh bilioni 236 zilitengwa kununulia dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi. 

Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi alisema upatikanaji wa dawa muhimu kwa mwaka 2016/17 iliongezeka kwa asilimia 50 ikilinganishwa na ya mwaka 2015/16. 

Alisema katika kipindi cha kuanzia Julai mwaka jana hadi Februari Lindi ilipokea Sh milioni 538 za dawa kupitia Bohari Kuu ya Dawa (MSD). 

“Hospitali ya Mkoa ilipokea Sh 195,328,186 za dawa na ilitumia Sh 127,171,700 kutoka fedha za uchangiaji kununulia dawa,” alisema. 

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwaagiza watendaji wa Halmashauri kwenda vijijini kuelimisha wananchi umuhimu wa utunzaji  mazingira ili kuliepusha Taifa na jangwa. 

Pia aliagiza maofisa kilimo kuacha kushinda ofisini na badala yake waende mashambani kuelimisha wakulima namna bora ya kulima kwa kufuata njia za kisasa ili kupata tija. 

Alitaka kila ofisa kilimo awe na shamba darasa litakalotumika kuelimisha wananchi.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo