Uganda yahamia bandari ya Dar es Salaam


Celina Mathew

SERIKALI ya Uganda imeamua kutumia usafiri wa maji kusafirisha bidhaa na huduma zake kutokana na unafuu kuliko njia ya reli inayoonekana kuwa aghali zaidi.

Katika uamuzi huo, Uganda imechagua bandari ya Dar es Salaam kuwa sehemu yake ya kusafirishia bidhaa na huduma kwa kuwa ni nafuu na salama zaidi kuliko bandari zingine.

Hatua hiyo inakuja wakati nchi hizo mbili zikitarajiwa kunufaika na bomba la mafuta kutoka Uganda hadi Tanga ambapo ushirikiano huo umeendelea kuleta manufaa kwa mawaziri wa sekta ya usafirishaji kuendelea na mazungumzo ya kuendeleza ukanda wa kati wa usafirishaji na uchumi endelevu.

Akizungumza Dar es Salaam jana wakati kusaini makubaliano katika usafirishaji kati ya nchi hizo mbili, Waziri wa Usafirishaji wa Uganda Henry Bagiire alisema Serikali yake inatamani kuboresha ukanda wa kati kama mkakati wa kuhakikisha wanafikia uchumi wa kati.

Alitaja maeneo ambayo yanahitaji utekelezaji kuwa ni pamoja na kuboresha kivuko cha mv Kaawa, kuandaa bandari za Bell na Jinja na kuifanyia matengenezo bandari ya Bukasa.

“Usafiri wa maji ndio chanzo kikuu cha kusafirisha bidhaa kirahisi, hivyo uchumi wa nchi yetu hautafanikiwa bila njia hiyo, hata ukingalia nchini ukitaka kusafirisha chai kwa reli unatumia dola milioni 120 kwa tani tena kwa ufanisi lakini kwa maji ni dola milioni 60,” alisema.

Alisema ukitumika usafiri wa maji kwa kiasi kikubwa utaokoa dola milioni 40 kwa mwaka na kwamba kwa mwaka 2003 ukanda huo ulihudumia tani 330,000 sawa na asilimia 30.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alisema kufanikiwa kwa njia hiyo ya Uganda kusafirisha bidhaa zake kupitia bandari ya nchini kutaleta ufanisi kwenye sekta hiyo.

“Uganda ni rafiki zetu, hivyo tunashirikiana nao kuhakikisha wanatumia bandari hii kwa kuwa itasafirisha mizigo kwa ufanisi kutoka Dar es Salaam-Mwanza hadi Kampala, kwa saa 24 tu,”alisema.

Alisema suala hilo likisimamiwa vizuri, mizigo ya nchi hiyo itafikishwa kirahisi na kwa muda mfupi na kuondoa urasimu wa wateja kupewa risiti nyingi na badala yake watapewa moja tu ya gharama zote.

Aliongeza kuwa pia utaleta faida kwa pande zote mbili, kwa kuwa ni wajibu kwa nchi hizo kutumia bandari za pande zote kwa kuwa ni ndugu kwenye masuala ya biashara.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Deusdedit Kakoko alisema kufanikiwa kwa makubaliano hayo, kutawezesha mizigo ya Uganda kusafirishwa kwa siku siku nne badala ya tano kupitia njia ya Mutukula.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo