Majaliwa akagua ujenzi wa daraja


Mwandishi Wetu, Lindi

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amekagua ujenzi wa daraja la Mto Lukuledi lenye urefu wa kilometa 30.45 likiunganisha mikoa ya Lindi na Mtwara na kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi huo. 

Amesema ujenzi wa daraja hilo unatakaogharimu Sh bilioni 5.4 ni mkombozi kwa wananchi wa mikoa hiyo hasa wilaya za Ruangwa na Masasi, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakishirikiana katika masuala ya kilimo na kijamii.  

Waziri Mkuu alisema hayo jana kwenye daraja hilo katika kijiji cha Nandanga alipowasili Ruangwa akiwa katika siku ya pili ya ziara yake ya kikazi ya siku nne mkoani Lindi. 

“Watu wengi wamepoteza maisha kwa kuliwa na mamba wakikatiza eneo hili. Ujenzi wa daraja hili ni muhimu, watu wengi wa Ruangwa wanavuka kufuata matibabu hospitali ya Ndanda, Masasi na wa Ndanda wanavuka kufanya shughuli za kilimo Ruangwa,” alisema Majaliwa. 

Waziri Mkuu aliomba wananchi wa maeneo hayo kuhakikisha wanatoa ushirikiano kwa mkandarasi anayejenga daraja hilo, ili aweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo na kumaliza mradi huo kwa wakati. 

Mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe aliipongeza Serikali kwa jitihada zake za kuwaletea wananchi maendeleo na kubadilisha maisha yao. 

Alisema mradi wa daraja hilo ni faraja kwa wananchi wa mikoa hiyo kwa kuwa eneo hilo ni makazi ya mamba, hivyo kukamilika kwake kutaokoa maisha ya watu na kurahisisha usafiri wa watu na bidhaa. 

Waziri Mkuu pia alisema changamoto ya upatikanaji huduma ya maji safi na salama katika vijiji vya Litama, Luchelegwa, Nandanga, Ipingo na Chiapi itakuwa historia baada ya kuunganishwa mradi wa maji wa Mbwinji. 

Alisema hayo alipozungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa Litama, Chiapi, Nandanga, Luchelegwa alipowasili Ruangwa. 

Majaliwa alisema Serikali inatekeleza kampeni yake ya kumtua mama ndoo, hivyo itahakikisha wananchi, hususan vijijini, wanapata huduma ya maji safi na salama umbali usiozidi meta 400. 

Waziri Mkuu pia alizindua zahanati ya Nandanga ambayo imejengwa kwa fedha za Mfuko wa Jimbo kwa Sh milioni 73.47 na kuwahakikishia kwamba  Serikali itawapelekea  wataalamu wa kutosha kuwahudumia.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo