Wavamizi wa reli wapewa miezi sita


Mwandishi Wetu

Reli
SERIKALI imetoa miezi sita kwa wakazi wa Mpanda mkoani Katavi kuondoka maeneo ya hifadhi za reli ili kupisha maboresho yanayoendelea kufanywa na Shirika la Reli Tanzania (TRL) kwenye miundombinu yake.

Agizo hilo la Serikali lilitolewa juzi na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngoyani akizungumza na wafanyakazi wa taasisi zilizo chini ya wizara yake mkoani Katavi ambapo alisema ni wakati sasa kwa wananchi kufuata sheria kwa kutovamia miundombinu hiyo.

“Ninatoa miezi sita kuanzia sasa, itakapofika Januari mwakani wananchi wote watakaokuwa ndani ya hifadhi ya reli watabomolewa nyumba kwa kuzingatia sheria zinazolinda miundombinu,” alisema Ngonyani.

Aidha, Ngonyani aliuagiza uongozi wa mkoa kusimamia wananchi kuhama na kuhakikisha kila aliyevamia miundombinu anabomoa nyumba yake kabla ya sheria kufuata mkondo wake.

Naibu Waziri aliwahadharisha wafanyakazi wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuzingatia maslahi ya Taifa wakati wa kutafuta zabuni.

Ngonyani pia alikagua barabara ya Kanazi-Kizi-Kibaoni (Km 76.6), Sumbawanga-Kanazi (Km 75) na kuiagiza TANROADS mkoa wa Rukwa kuweka mizani kwenye barabara zinazojengwa, ili kudhibiti magari

makubwa yanayozidisha uzito na kusababisha uharibifu kwa barabara za mkoa huo.

“Ni wakati sasa wanaotoa huduma za usafirishaji mizigo kufuata  sheria na kubeba mzigo wa uzito stahiki, kwa sababu madereva hao hao wakienda nchi jirani wanafuata sheria kwa umakini, SUMATRA simamieni utoaji wa leseni kwa magari ya abiria na mizigo kwa kuzingatia uzito wa magari ili kuziweshesha barabara zetu zidumu,” alisema Ngonyani.

Meneja wa TANROADS wa Mkoa wa Rukwa, Msuka Mkina alimhakikishia   Ngonyani kwamba wakala wake utahakikisha mizani inawekwa sehemu za barabara ili kubaini magari yanayozidisha uzito na kuyachukulia hatua za kisheria.

Ngonyani anafanya ziara ya kukagua miundombinu ya barabara, viwanja vya ndege, ujenzi wa nyumba za viongozi, huduma za mawasiliano ya simu   na madaraja katika mikoa ya Katavi na Rukwa.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo