‘Dude’ vyeti feki kuigeuka Serikali


Mwandishi Wetu

Waziri Angella Kairuki
SERIKALI imejiweka katika hatari ya kudaiwa mabilioni ya fidia na watumishi wa umma 450 waliobainika kutangazwa kimakosa kuwa wamiliki wa vyeti feki.

Wakizungumza na mwandishi wa JAMBO LEO kwa masharti ya kutotajwa gazetini jana, baadhi ya wanasheria waliweka wazi kuwa ni haki kwa watu hao kuishitaki Serikali kwa mujibu wa sheria ya kudai fidia baada ya kukashifiwa.

Mmoja wa wanasheria hao alisema inafahamika kuwa mtu anayefanyiwa hivyo na baadaye kubainika kuwa haikuwa hivyo, anapata athari.

“Hilo jambo liko wazi na hata Serikali inafahamu kuwa haki ya kushitaki, mtumishi anayo labda kama wataogopa kuishitaki Serikali ambayo inawalipa mshahara,” alisema.

Mwanasheria mwingine alisema kumwita mtu ana cheti feki ni kumdhalilisha, lakini kwa kuwa imethibitika vinginevyo, mwajiri ambaye ni Serikali, anapaswa kumrudisha kazini na kumpa stahiki zake zote.

“Huyo anatakiwa arudishwe kazini na kama mwajiri wake ataona hayupo tayari kufanya hivyo, anatakiwa ampe stahiki zake zote na huo ndio utaratibu kisheria.

“Anaweza kushitaki kwa kudhalilishwa, lakini hata akishitaki mwajiri atatakiwa kumrudisha kazini na kama hataki kuendelea kufanya naye kazi, anatakiwa kumlipa stahiki zake zote kutokana na kumchafulia jina,” alisema mwanasheria huyo.

Juzi, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Utawala Bora, Dk Laurian Ndumbaro alisema awali watumishi wa umma  9,932 walibainika kukutwa na vyeti feki, katika uhakiki wa vyeti vya kidato cha nne, sita na ualimu uliofanywa na Serikali.

Alisema baada ya kutangazwa kwa orodha ya watumishi hao, watumishi 1,050 walikata rufaa na baada ya kupitia rufaa hizo, watumishi 450 walishinda rufaa hizo.

Alifafanua kuwa katika rufaa zilizokubaliwa, ilibainika kuwa baadhi ya watumishi walikuwa wakitumia majina ya waume zao baada ya kuolewa, ambayo yalitofautiana na majina yaliyo kwenye vyeti.

“Bahati mbaya Watanzania wanapoolewa hutumia majina mawili ya waume zao, badala ya moja. Hivyo ilileta usumbufu wakati wa uhakiki baada ya vyeti vyao kuonesha majina tofauti,” alisema.

Wengine walioshinda rufaa ni ambao majina yao ya kidato cha nne, yalikuwa tofauti na ya kidato cha sita, kwa kuwa kidato cha nne hawakutumia majina ya kati kama ya kidato cha sita, lakini baada ya kujieleza walikubaliwa rufaa na kurejeshwa kwenye utumishi wa umma.

Wengine ni walioonekana kuwa na karatasi za vyeti ambazo si sahihi, lakini matokeo ni sahihi na walisoma kwenye shule husika na baada ya kuhojiwa na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), walionekana walipata vyeti shuleni kwao, lakini karatasi zilizotumika hazikuwa sahihi kutokana na wao kuchelewa kuchukua vyeti vyao kwa miaka mingi.

“Hawa wa kundi hili hawakuwa na lengo la kubadilisha matokeo, hivyo ilionekana wanastahili kurejeshwa kwenye utumishi wa umma, kwa kuwa walipewa vyeti ambavyo havikubadilishwa matokeo,” aliongeza.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo