Serikali, wawekezaji wakaa meza moja


Mwandishi Wetu

KAIMU Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa James Mdoe amefanya mazungumzo na uongozi wa kampuni za Uranium One na Mantra Tanzania wanaomiliki leseni ya uchimbaji madini ya urani kwenye eneo la Mto Mkuju Kusini mwa nchi.

Mantra ni sehemu ya kampuni ya Uranium One na kampuni ya kimataifa ya madini ya ROSATOM-ya Shirikisho la Serikali ya Urusi ya Nishati ya Nyuklia.

Kikao hicho kilijadili ushirikiano kati ya Tanzania na kampuni hizo, kuporomoka kwa bei ya urani kwenye soko la dunia na kampuni hizo kushirikiana na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) katika miradi ya madini.

Rais wa Uranium One Group, Vasility Konstantinov aliishukuru Serikali kwa ushirikiano inaoendelea kuutoa kwao ili kuhakikisha kuwa lengo la kampuni la kuendeleza mradi wa uchimbaji madini ya urani nchini linafanikiwa.

Konstantinov pia alikanusha habari zilizoandikwa na baadhi ya magazeti nchini hivi karibuni kuwa MANTRA Tanzania imesitisha uchimbaji wa urani kwenye leseni yao iliyoko eneo la Mto Mkuju moja ya sababu ikiwa ni mabadiliko katika Sheria ya Madini.

Alisisitiza kuwa maombi ya Mantra Tanzania ya kupata  ridhaa ili kusitisha uchimbaji madini ya urani kwa muda wa miaka mitano, yanatokana na kushuka kwa soko la madini duniani na kwamba suala hilo halijaiathiri kampuni hiyo pekee, bali hata baadhi ya kampuni.

“Mradi huu ni muhimu kwa ROSATOM, hatutaki kuondoka, tunataka kuendelea kuwa hapa, tuendeleze ushirikiano mpaka hapo bei ya urani itakapopanda ili tutekeleze mradi kwa manufaa ya pande zote mbili,” alisema Konstantinov.

Aliongeza kuwa kampuni hiyo itaendelea kuendeleza miradi mingine ya kijamii mkoani Ruvuma, na tayari wamejadiliana na uongozi wa mkoa kuona jinsi watakavyoshiriki kwenye miradi hiyo ya kijamii.

“Hii inaonesha kuwa mradi huu ni muhimu kwetu na tunataka kuuendeleza mapema iwezekavyo, lakini kikwazo sasa ni kuporomoka kwa bei ya urani,” alisema Konstantinov.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mantra Tanzania, Frederick Kibodya alisema   uwasilishaji wa maombi ya kusitisha uchimbaji urani serikalini, haumaanishi kuwa kampuni hiyo itasimamisha shughuli zake zote nchini.

Alisema kampuni hiyo itaendelea kufadhili miradi ya kijamii na imeanza mazungumzo na STAMICO ili kushirikiana kuendeleza miradi ya uzalishaji makaa ya mawe na dhahabu.

Profesa Mdoe aliwaeleza watendaji wa kampuni hizo kuwa maombi yao la usitishaji uchimbaji madini ya urani nchini yamefika serikalini na kwamba yatatolewa uamuzi muda mwafaka ukifika.

Kuhusu nia ya kampuni hiyo kushirikiana na STAMICO kwenye miradi ya  madini, Profesa Mdoe aliikaribisha kwani lengo la Serikali ni kukaribisha wawekezaji nchini wenye nia njema ya kuendeleza miradi itakayoleta tija kwa Taifa.

Kuhusu mabadiliko katika Sheria ya Madini, Profesa Mdoe alisema lengo ni kuhakikisha nchi inafaidika na rasilimali zake na kama mwekezaji anafuata matwaka ya nchi katika uwekezaji, atakuwa hana sababu ya kuogopa mabadiliko.

“Mabadiliko ya Sheria ya Madini ni kwa ajili ya kunufaisha pande zote na  si kunyanyasa mwekezaji, kama mwekezaji anakuja kwa nia nzuri hana sababu ya kuogopa,” alisema Profesa Mdoe.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo