Mganda, Mtanzania kizimbani kwa uhujumu uchumi


Grace Gurisha

RAIA wa Uganda, Edwin Gusongoirye (30) na mfanyabiashara, Steven Simon (45) wamefikishwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na tuhuma za uhujumu uchumi kwa kuisababishia Serikali hasara ya Sh milioni 210.2.

Gusongoirye ambaye pia ni mfamasia na Simon walifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi, Godfrey Mwambapa.

Akisoma mashitaka hayo, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Nassoro Katuga alidai kuwa kati ya Machi 6 na Juni 22, Dar es Salaam, washitakiwa walitengeneza mfumo wa kutumia huduma za mtandao kukwepa kodi ya kupokea na kusambaza mawasiliano bila kibali.

Pia kati ya Machi 6 na Juni 22, mwaka jana washitakiwa hao waliendesha mfumo wa kupokea na kusambaza mawasiliano ya kimataifa bila leseni ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Katuga alidai katika mashitaka ya tatu kuwa katika tarehe na mwaka huo huo, Gusongoirye na Simon waliingiza vifaa vya mawasiliano nchini ambavyo ni makasha matatu ya simu bila kibali cha TCRA.

Katika mashitaka ya nne, ilidaiwa kuwa kabla ya Machi, 2012 washitakiwa walisimika vifaa vya mawasiliano zikiwamo kompyuta mpakato mbili aina ya Dell na Hp bila kibali.

Pia ilidaiwa kuwa washitakiwa walitumia vifaa vya mawasiliano ambavyo havijathibitishwa kwa lengo la kupokea na kusambaza viashiria vya mawasiliano bila kuthibitishwa na TCRA.

Katuga alidai pia kuwa Machi 6 na Juni 22, kwa makusudi na kwa pamoja waliisababishia Serikali hasara ya Sh milioni 210.2.

Washitakiwa hawakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza mashitaka ya uhujumu uchumi na kwamba haiwezi kutoa dhamana, kwani mashitaka hayo ni ya zaidi ya Sh milioni 10 ambayo wanatakiwa kuomba Mahakama Kuu.

Katuga alidai kuwa upelelezi wa shauri hilo haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kesi kutajwa na Hakimu Mwambapa aliiahirisha   hadi Julai 25, itakapotajwa.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo