Wakazi Kigamboni kuchangia uzoaji taka


Suleiman Msuya

Daraja la Kigamboni
WAKAZI wa Wilaya ya Kigamboni, wataanza kulipia Sh. 3,000 kwa mwezi kwa ajili ya uchangiaji uzoaji taka ikiwa ni mikakati ya wilaya hiyo kuwa na mazingira safi.

Hayo yamesemwa na mkuu wa wilaya hiyo, Hashimu Mgandilwa wakati akizindua mpango wa uchangiaji uzoaji taka kila kaya huku akibainisha kuwa kiasi hicho ni sawa na kutoa sh. 100 kila siku kwa kaya.

Mgandilwa alisema mpango huo utasaidia kupunguza suala la uchafu katika wilaya hiyo na gharama zake ni nafuu tofauti na awali ambapo kaya moja kwa kata ya Kibada walilazimika kulipa kiasi cha Sh. 20000 mpaka 40,000 jambo ambalo ni changamoto kwa wakazi hao.

Alisema Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli imedhamiria kurahisisha maisha kwa wananchi wake, hivyo ni imani yake kuwa kila mwananchi ataweza kuchangia kiasi hicho cha sh. 3,000.

“Mradi huo utasaidia changamoto iliyojitokeza ya baadhi ya watu kutupa taka kwenye fukwe ya bahari, lakini pia utaratibu huu utasaidia kukabiliana na magonjwa ambayo yanazulika,” alisema.

Aidha, mkuu huyo wa wilaya amewaomba wananchi katika kaya mbalimbali kutunza taka zinazozalishwa majumbani mpaka magari ya mradi yatakapokuja kuzichukua zikiwa katika mazingira mazuri.

Alisema tafiti zinaonesha kuwa chanzo kikubwa cha magonjwa ya milipuko kinatokana na kuzagaa kwa takataka kwenye mazi ya watu hivyo ni jukumu la kila mwananchi kuhakikisha anakuwa mlinzi kwa mwenzake kuhusu utupaji taka.

Mgandilwa alisema mkakati wa halmashauri ni kuhakikisha mradi huo unakuwa wa uhakika na kuwa magari nane ambayo yamepatikana kwa sasa yatazunguka kata zote.

“Halmashauri haina uwezo wa kutoa msisitizo kila wakati ili watu watunze mazingira hivyo ni jukumu la Wanakigamboni kutunza mazingira kwa faida yetu,” alisema.

Alisema utaratibu huo utawahusu hadi wamiliki wa hoteli na taasisi mbalimbali ambao wao wamewekewa kiasi ambacho ni nafuu kwao.

Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Steven Katemba ameeleza kuwa mradi huo utawanufaisha vijana zaidi ya 134 na utaanza kwa kata tano ikiwemo Kigamboni, Mjimwema, Tungi, Kibada na Vijibweni.

Alisema mipango ya halmashauri ni kukamilisha ujenzi wa dampo la Lingato ambapo bilioni moja imetengwa na halmashauri ya Jiji kwa ajili ya ukarabati wa dampo hivyo ndani ya miezi kadhaa ukarabati utakwisha na taka hazitakuwa zinapelekwa huko.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo