Serikali yachunguza akaunti za watumishi


Uchunguzi wa Jambo Leo kwa takriban wiki mbili, umebaini Serikali ‘kudukua’ akaunti hizo kwa watumishi wake wote kwenye wizara, taasisi na halmashauri zote nchini ili kubaini miamala hiyo.

“Sikia, sisi watumishi hali inazidi kuwa ngumu, Serikali sasa imeanza hata kuchunguza akaunti za watumishi wake,” alisema mtoa habari wetu kutoka moja ya wizara nyeti serikalini. Alipoulizwa lengo la kufanya hivyo, alisema: “Serikali inataka kudhibiti mapato yasiyo halali kwa watumishi wa umma.”

Uchunguzi umebaini kuwa Serikali inalenga kugundua watumishi ambao akaunti zao zina fedha nyingi kuliko kipato chao cha kawaida au zinapitisha fedha kutoka au kwenda akaunti zinazotiliwa shaka, hasa kuhusu ufisadi, pia mishahara hewa.

Hata hivyo, taarifa zinaonesha kuwa sheria za kibenki haziruhusu mtu asiye mwenye akaunti husika kuchunguza akaunti ya mtu bila idhini kwani ni kosa kisheria.

Kwa mujibu wa Mwanasheria, Aloyce Komba, taarifa za akaunti ya mtu ni siri kati yake na benki husika.

"Haki hiyo itageuzwa kwa amri ya Mahakama, au akaunti itachunguzwa kwa amri ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ambayo sasa imepewa mamlaka ya kufanya hivyo," alisema.

Aliongeza: "Pia hilo linaweza kufanyika kwa ruhusa ya Meneja wa Benki husika, lazima uchunguzi huo uendane na sharia au mamlaka, kama nilivyosema. Kamishna wa Maadili anaweza kuagiza hilo iwapo atabaini viongozi waliowasilisha hati za kiapo cha maadili na mali zinatia shaka, vinginevyo itakuwa ni kosa."

Alisema uchunguzi wa akaunti binafsi ya mtumishi hufanyika kwa kutumia pia Sheria ya Udhibiti wa Fedha Haramu. Hata hivyo, chanzo cha habari kilieleza kuwa mbali na hatua hiyo, Serikali pia imepiga marufuku watumishi wake kupokea zawadi au fedha kama shukrani kutoka kwa watu wanaohudumia.

Kwa mujibu wa uchunguzi huo, mfanyakazi atakayebainika kupokea fedha au zawadi kutoka kwa mtu au taasisi aliyoihudumia na kubainika, atachukuliwa hatua za kinidhamu.

Habari zinapasha kuwa kwa hatua hiyo, watumishi wa Serikali wanatakiwa kuweka wazi kwa kutoa taarifa kwa wakuu wao wa idara iwapo watapewa fedha au zawadi kutokana na kazi wanazofanya.

"Tumeambiwa ni marufuku kupokea zawadi yoyote hata fedha, tukitaka kufanya hivyo tutoe taarifa kwa wakubwa na kueleza tumepewa nini au kiasi gani," alisema mmoja wa watumishi katika Wizara ya Ardhi.

Mtumishi mwingine alisema: "Si kuzuiwa kupokea zawadi tu na fedha tu, Serikali ya Awamu ya Tano imetusainisha wote hati za kiapo cha maadili, kina mambo mengi pamoja na hayo."

Mwandishi wa gazeti hili alimtafuta Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dk Servacius Likwelile kuzungumzia suala hilo Jumapili iliyopita, lakini akasema hayupo tayari kuzungumza kwa sababu yuko nyumbani amepumzika na kumtaka mwandishi amtafute ofisini siku inayofuata. 

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dk. Servacius Likwelile alikanusha kuwepo kwa uhakiki huo akisema: “Serikali haina mpango wa kufanya uhakiki wa miamala ya fedha kwenye akaunti za watumishi wa umma na idara zake nchini."

Akizungumza na Jambo Leo jijini Dar es Salaam jana, Dk Likwelile alisisitiza: ìHakuna uhakiki unaofanywa na Serikali kimya kimya, kama utakuwapo vyombo vya habari vitajulishwa ili Watanzania wafahamu."

Hata hivyo, habari za uhakika kutoka ndani ya Serikali zinaeleza kwamba miamala ya fedha kwenye akaunti za watumishi wa umma na idara zake inahakikiwa. "Unafanyika kupitia manispaa na halmashauri zote nchini.

Lengo la uhakiki huo ni zuri. Ni kuhakikisha mishahara inamfikia mlengwa na kuepuka kulipa watumishi hewa kama ilivyokuwa awali ambapo mtu mmoja alimiliki akaunti zaidi ya moja," alisema mmoja wa watendaji wa Wizara ya Utumishi aliyeomba kuhifadhiwa jina kwa kuwa si msemaji.

Hata hivyo, alisema kinachosubiriwa ni mrejesho kamili kutoka kwa wakurugenzi wa Halmashauri na Manispaa na kwamba taarifa husika zitatumwa Wizara ya Fedha na Mipango kwa ajili ya hatua zaidi za kiserikali.


"Kazi inafanyika, lakini bado mrejesho wa utekelezaji kutoka kwa wakurugenzi wa manispaa na halmashauri haujawasilishwa Serikali Kuu kwa maana ya Wizara ya Fedha na Mipango, naamini hilo linasubiriwa na wahusika." alieleza mtendaji huyo.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo