Muhongo: Serikali imekusudia kufuta umaskini



WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, amesema Serikali ya Awamu ya Tano imekusudia kufuta umaskini kwa Watanzania.

Pia aliwahimiza wananchi waliopitiwa na mpango wa umeme vijijini kuunganishwa na nishati hiyo ili kuondokana na matumizi ya vibatari.

Muhongo alisema juzi kuwa wananchi wanatakiwa kuchangamkia fursa ya Mradi wa Rea hasa ikizingatiwa kwamba gharama ya kuunganishiwa umeme ni Sh. 27,000. Alisema mwisho wa malipo ni Oktoba 30, mwaka huu.

Katika mazungumzo yake na wananchi wa Kata ya Dindira, Tarafa ya Bungu, Prof. Muhongo alielezea kushangazwa kwake na mwamko mdogo wa wananchi kuunganishiwa umeme licha ya kutozwa gharama ndogo.

Alisema serikali imejipanga kuwakwamua wananchi wake ambapo wakitumia fursa ya nishati ya umeme vijijini kujianzishia miradi ya uzalishaji mali wataimarisha uchumi wao. "Ndugu zangu hali ikiendelea hivi haitawezekana Mradi wa Rea awamu ya tatu kuja tena wataangalia kwenye ëspeedí kubwa, hivi sasa tu hamjaweza kumaliza nafasi zenu waliojiunga ni wateja 470 wakati matarajio ni zaidi ya wananchi 1,200," alisema.

Muhongo alimtaka Meneja wa Tanesco Wilaya ya Korogwe, Dominic Mwikanu kufika Dindira kuwaelimisha wananchi ili kuunganishiwa umeme huo. Alisema serikali imejipanga kufikisha nishati ya umeme kwenye vijiji vyote ambapo Rea awamu ya tatu mbali na kufika vijiji vitakavyokuwa vimeainishwa kipaumbele kitatolewa kwa nyumba za ibada, shule, zahanati, nyumba za biashara na vyama vya siasa.

Katika ziara hiyo, alitumia fursa hiyo kukanusha uvumi uliozagaa kwa wananchi kuwa Rea ni mradi ambao umeletwa na Rais wa Marekani, Barack Obama.

Alisema mradi huo unatokana na kodi za wananchi na unaendeshwa na serikali yao. Muhongo alitoa ufafanuzi huo baada ya Mbunge wa Korogwe Vijijini, Stephen Ngonyani kumweleza kwamba baadhi ya watu wamekuwa wakimkebehi kuwa nishati hiyo ya umeme haikufikishwa maeneo yao kwa nguvu za serikali.

"Huu si umeme wa Obama, ni fedha za walipa kodi, kila uchao mbunge wenu amekuwa akijitahidi kunikumbusha kuhusu umeme, safari ya umeme nimeanza naye na ningependa tumalize wote, msimuangushe," alisema Prof. Muhongo.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo