Kingunge aomba marais waokoe jahazi

Na SharifaMarira

MWANASIASA Mkongwe Nchini, Kingunge Ngombale Mwiru amewaomba viongozi wakuu wastaafu wa kitaifa kuzungumza na Rais John Magufuli kuhusu  mgogoro uliopo kati ya Chama cha Demokrasia na Maendelo (Chadema) na Serikali ili kuepusha uvunjifu wa amani.

Kingunge alisema hayo jana akieleza hali iliyopo sasa ya mvutano kati ya Serikali na Chadema kupitia Operesheni ya Kutetea Demokrasia (Ukuta) iliyopangwa kufanyika Septemba Mosi, busara za wazee hao zinahitajika kwa kukutana na Rais Magufuli kumshauri isipokuwa, lakini bila kuwemo Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete.

Ametoa kauli hiyo zikiwa zimesalia siku saba kabla ya kufanyika kwa Opereseni Ukuta, wakati alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya kisiasa nchini na kauli ya Rais Magufuli kupiga marufuku mikutano yote ya kisiasa ambayo alidai ndiyo iliyoleta mgawanyiko na  ni uvunjifu wa katiba na kuvinyima haki vyama vya siasa.

“Nawaombeni wazee wa nchi hii, Kikwete hastahili katika hili, zungumzeni na mzee mwenzenu Magufuli kwa haraka zaidi kwani zimebaki siku saba pekee ifanyike Opresheni Ukuta, ambayo itaumiza vijana wa kitanzania na amani itatoweka. Haki isipotendeka hakuna amani daima,” alisema Kingunge.

Alifafanua kwamba Kikwete hastahili kuwepo katika kundi hilo akimtaja ndiye aliyelifikisha Taifa lilipo sasa katika ombwe la uongozi kwa kuacha waliokuwa na uwezo bila kuwapa nafasi kuongoza.

Aliongeza: “Wazee wenzangu ambao wote mliapa kwa kauli ya kuilinda,kuihifadhi na kuitetea katiba ya nchi,msikae kimya hivi sio sawa,lazima tujitokeze tuhesabiwe,hatuwezi kubaki nyuma tukubaliane kuingilia kati jambo hili tusisubiri yatokee matatizo ndiyo tuzungumze.”

Kingunge alisema jambo kubwa ambalo wazee wanapaswa kuomba kuonana na Magufuli ni kumuomba aitishe kikao cha mazungumzo na Chadema na kwamba baada ya kufanya hivyo watakigeukia chama hicho kuwataka wasitishe Ukuta ili kuepusha shari na uwezekano wa kuvuja damu.

“Hakuna sababu ya kumwaga damu wakati wazee wenye busara tupo,ingekuwa Chadema wanavunja katiba na sheria serikali ingekuwa inafanya vyema kuwashikisha adabu lakini sasa serikali inashindana na watu wanaotetea haki na katiba ambao ndio kundi kubwa”alisema Kingunge

Alisema kauli ya Magufuli ndiyo iliyosababisha mgawanyiko wa maoni katika jamii wapo waliomuunga mkono lakini kundi kubwa halijakubaliana na amri yake hivyo yanayotokea sasa yanatokana na kauli yake ni vyema wazee kutoyafumbia macho ili nchi ibaki salama.

Alisema endapo wastaafu hao hawatafanya jitihada hizo jambo lolote linaweza kutokea na ni wazi kwamba Amani itaponyoka kutokana na hali ya kisiasa kuwa tete ,ina utata na ni ngumu.

Alisema ni vyema wazee wakakumbuka kuwa wajibu walio nao kwa watanzania ni kutumia busara zao kama walivyokula viapo na kwamba jambo hilo sio la Chadema ni la watanzania wote.

“Kama tunavyoona kuna pande mbili zinazovutana upande mmoja unanoa mapanga,visu na silaha za moto na kufanya mazoezi wazi wazi ili kuwakomesha wengine lakini ukiangalia raia wa kawaida wanalilia Amani bila kujua kwamba haiwezi kupatikana bila haki”alisema

Hata hivyo Kingunge alisema nchi kwa sasa ina ombwe la uongozi lakini wapo viongozi wengine waliopo nje ya serikali ambao wana uwezo wa kuongoza na hawajapewa nafasi na kwamba kuna umuhimu kwa watu wanaopewa madaraka kuzijua na kuziheshimu haki za kisiasa.

Alisema tatizo kubwa lililopo sasa binadamu wanaishi kwa chuki na uhasama ndiyo maana Amani inaweza kutoweka na kwamba mungu anawasaidia watu wanaojisaidia hivyo wanaoomba wananchi kuombea Amani ya nchi ni vyema wakawa wa kwanza kusimamia,kulinda na kutetea haki.

Mwisho.

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo