Si sahihi CCM, IGP, AG kukataa wito wa Tume



Na Malisa Godlisten

KWA muda wa miezi kadhaa sasa kumekuwa na changamoto ya kisiasa kati ya chama tawala, vyama vya upinzani, jeshi la polisi na ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali.

Changamoto hiyo inatokana na hali ya sintofahamu iliyoibuka juu ya utendaji na shughuli za vyama vya siasa nchini. Mgogoro huu ulianza baaada ya Rais John Pombe Magufuli kupiga marufuku mikutano ya kisiasa na maandamano akitaka wananchi na wafuasi wa vyama vya siasa kujiegemeza zaidi katika shughuli za maendeleo badala ya mikutanoi ya kisiasa au maandamano.

Agizo hili la Rais lilipokelewa na vyombo vya dola ambapo Jeshi la Polisi lilipiga marufuku mikutano ya kisiasa, maandamano hata vikao vya ndani kwa madai kuwa shughuli za kisiasa ni hadi mwaka 20120. Chama cha Demokrasi na maendeleo (CHADEMA) na vyama vingine vinavyounda UKAWA vikajikuta vimekua wahanga wa kwanza wa agizo hilo. Walizuiwa kufanya mikutano ya hadhara, mikutano ya ndani wala semina na vikao kazi vya chama.

Wakati vyama vya upinzani vikizuiwa kufanya shughuli zao za kisiasa, Chama Cha Mapinduzi kinaendelea na shughuli zake ikiwa ni pamoja na Rais Magufuli kutumia mikutano mbalimbali ya hadhara kukinadi chama chake. Bila shaka hili ndilo linalofanya vyama vya upinzani kuona kuwa wanafanyiwa uonevu lakini chama cha mapinduzi kinapendelewa.

Tume hiyo iliandaa mkutano utakaohusisha taasisi sita, ikiwamo Jeshi la Polisi lililozuia mikutano, CCM inayoendesha Serikali na Chadema inayopinga maamuzi ya Serikali kwa madai kuwa yanakandamiza demokrasia na kukiuka misingi ya utawala bora.

Waliopaswa kuhudhuria kikao hicho ni makatibu wakuu wa vyama hivyo, Abdulrahman Kinana (CCM), Vincent Mashinji (Chadema) na Ernest Mangu (Mkuu wa Jeshi la Polisi), Jaji Francis Mutungi (Msajili wa Vyama vya Siasa), George Masaju (Mwanasheria Mkuu wa Serikali) na Katibu mkuu wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD). Mkutano huo uliitishwa na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Bahame Nyanduga ambapo ulipaswa kufanyika jijini Dar es Salaam.

Kisheria Tume ya Haki na Utawala Bora ina jukumu la kuhamasisha hifadhi ya haki za binadamu, kuchunguza jambo lolote, kutoa ushauri kwa Serikali na vyombo vingine vya umma na kuchukua hatua za kukuza, kuendeleza, usuluhishi na suluhu miongoni mwa watu na taasisi.

Lakini katika hali ya kushangaza Chama cha mapinduzi (CCM), Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) na Mwanasheria Mkuu (AG) hawakutokea kuhudhuria mkutano huo wa usuluhishi ulioitishwa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kumaliza mvutano ulioibuka kati ya vyombo vya dola na Chadema.

Hatua hii ya vyombo vya dola pamoja na CCM kushindwa kuhudhuria mkutano huo ni dalili kuwa hawako tayari kutafuta utatuzi wa mgogoro huo. Hii inaweza kuwa hatua mbaya katika ukuaji wa demokrasia nchini.

Jeshi la Polisi limekuwa likijinasibu kila mara kuwa ni walinzi wa usalama wa raia na mali zao. Sasa mbona wanaona dalili za usalama wa raia kuharibika na hawataki kuchukua hatua? Au wanasubiri hadi September mosi ndipo waanze kuchukua hatua? Kwa nini Polisi hawataki kuzuia mgogoro (proactive) badala yake wanataka mgogogro utokee ndipo wahangaike kuutatua (reactive)? Polisi wamekuwa wakizuia matukio mbalimbali ya kijamii kwa taarifa za kiitelijensia. Je hawajapata taarifa za kiintelijensia kuwa Septemba mosi hali ya usalama inaweza kuzorota kama wasipochukua hatua? Sasa kwa nini wamekataa kushiriki katika mkutano wa usuluhishi? Wanapenda kuona mgogoro huu ukiendelea? Ikiwa CHADEMA pekee ndio waliotuma uwakilishi katika mkutano huo wa usuluhishi, ina maana kuwa ni CHADEMA pekee wenye dahamira ya kweli ya kutafuta suluhu ya mgogoro huu. Je CCM Jeshi la Polisi na Ofisi ya Mwanasheria mkuu ambao ni wadau wakuu wa mgogoro huu hawataki kuona mgogoro huu ukiisha? Kitendo cha kutohudhuria mkutano wa usuluhishi ni dalili kuwa kuna agizo lililowazuia kushiriki. Haiwezi kuwa bahati mbaya. Bila kukutana hakuna lolote linaloweza kufanyika ili kutafuta suluhu. Wataalamu wa utatuzi wa migogoro wanaeleza kuwa ikiwa pande zinazozozana zimekubali kukutana ni dalili nzuri ya kutafuta suluhu. Upande usiokubali kushiriki hauko tayari kuona mgogoro ukimalizwa. Hii ni kusema kwamba CCM, IGP na AG hawapo tayari kumaliza mgogoro wa kisiasa uliopo. Hii haiwezi kuwa habari nzuri katika mchakato wa ukuaji wa demokrasia nchini. Na ni aibu kwa chama tawala na taasisi nyeti kama jeshi la polisi na ofisi ya mwanasheria mkuu kukataa kushiriki katika mkutano wa usuluhishi.

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo