Kasi ya JPM yapaisha mapato Utalii


Mwandishi Wetu

KASI ya Rais John Magufuli kuhakikisha Tanzania inajitegemea kwa kila mtu kulipa kodi, imeanza kulipa baada ya takwimu kuonesha, kwamba watalii wameongezeka na hivyo kuongeza mapato serikalini.
Ukweli huo ulitolewa jana Dar es Salaam na Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe alipokuwa akizungumzia mikakati iliyotekelezwa na Wizara yake.
“Pamoja na kelele za sekta ya utalii baada ya Serikali kuanza kutoza Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) nakuhakikishia hivi sasa watalii wameongezeka na mapato yamekua kwa asilimia 22 zaidi,” alisema Waziri Maghembe.
Alitanabahisha kuwa tofauti na mtazamo wa wadau wa sekta ya utalii, ongezeko la kodi hiyo halijaathiri watalii wengi hasa ikizingatiwa kuwa Tanzania inabaki kuwa na vivutio vya kipekee duniani.
“Nchi yetu ina vivutio vingi ambavyo havipo nchi nyingine. Hii ikijumlishwa na amani na utulivu nchini, hakuna mtalii atakayeshindwa kugharimia ongezeko la dola nane,” alisema Waziri.
Alitumia muda huo kueleza kuwa utafiti wake katika nchi za nje unaonesha balozi za Tanzania zinaongoza kwa kutoa viza kwa watalii ikilinganishwa na nchi za ukanda wa Afrika Mashariki hasa katika miji mikubwa kama ya Berlin, Ujerumani.
Akizungumzia vita dhidi ya ujangili, Waziri Maghembe alisema juhudi za Serikali kuwekeza kwenye mafunzo na vifaa vya kisasa zimezaa matunda pia baada ya ujangili kupungua nchini kwa kiasi kikubwa.
Alisema tayari watuhumiwa wakubwa wa mtandao wa ujangili wamekamatwa na baadhi wamehukumiwa vifungo jela.
Alimtaja mmoja wa watuhumiwa wakubwa wa mtandao huo kuwa ni raia wa kigeni ajulikanaye kwa jina la ‘Malkia wa Pembe za Ndovu’ ambaye naye yuko mahabusu kwa sasa.
“Katika vita hii tumeamua kuuchukulia ujangili kama ugaidi au uhujumu uchumi. Tumekamata majangili wakubwa na wafadhili wao na bado vigogo zaidi tunaendelea kuwafuatilia na muda wowote tutawakamata,” alisema.
Aliongeza kuwa Serikali pia imepiga marufuku uvunaji wa mazao ya misitu hasa magogo bila leseni na atakayefanya hivyo atakamatwa, mali na gari husika vitataifishwa na wahusika kufikishwa mahakamani.
Takwimu za kuongezeka watalii nchini zinaipa nguvu Serikali ya Rais Magufuli kwa sababu tangu alipoingia amekuwa akisisitiza umuhimu wa kukusanya kodi ili nchi ijitegemee.
Tofauti na mtazamo huo, baadhi ya watu wamekuwa hawaamini kama hilo linawezekana.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo