Polisi wanne wauawa wakilinda benki



Edith Msuya na Edith Msuya

WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi imesema tukio lilitokea maeneo ya Mbagala Mbande, Wilaya Temeke la polisi kuvamiwa na majambazi ambapo askari wanne waliuawa na raia wawili kujeruhiwa ni shambulizi dhidi ya askari polisi, wakidai kuna viongozi wa kisiasa wanaohusika na tukio hilo.

Mbali na kauli hiyo, jeshi hilo limepiga marufuku mikutano yote ya ndani ya vyama vya siasa ya kiutawala, kiutendaji  hata ya harusi likieleza mikutano hiyo ina viashria vya moja kwa moja kuhamasisha vurugu, hatimaye kuvunja sheria za nchi.

Akizungumza jana Dar es Salaam, Kamishna Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Nsato Mssanzya alisema: “Ni dhahiri wahalifu hao walikuwa na kusudio moja tu la kuwashambulia askari polisi. Wapo viongiozi wa kisiasa ambao wamesikika katika majukwaa ya kisiasa wakihamasisha wafuasi wao wawashambulie askari wa Jeshi la Polisi.”

Licha ya kuwahusisha baadhi ya viongozi wa kisiasa na tukio hilo Mssanzya alisema tukio hilo ni la uhalifu katika mazingira ya ulipizaji kisasi

Aliwataja askari waliouawa katika tukio hilo kuwa  ni E.5761 CPL Yahaya, F.4660 CPL Hatibu, G.9524 PC Tito na G.9996 PC Gastone huku waliojeruhiwa wakiwa ni Ally Chiponda na Aziz Yahaya wote wakazi wa Mbade.

Alisema katika tukio hilo majambazi hayo yalifanikiwa kupora silaha mbili aina ya SMG na risasi 60 na hakuna fedha au mali ya benki iliyoibwa au kuharibiwa.

“Kutokana na majambazi hayo kutochukua kitu chochote, ni dhahiri kuwa wahalifu hao walikuwa na kusudio moja tu la kuwashambulia askari polisi,”alisema Kamishna Mssanzya.

Kwa mujibu wa Kamishna Mssanzya, baada ya tukio hilo baadhi ya watu waliandika mitandaoni kubeza na kukejeli mazoezi ya kawaida yanayofanywa na Jeshi la Polisi huku wengine wakiandika ujumbe wa kushabikia tukio hilo la kuuawa kwa askari polisi.

“Wengine walidiriki kuandika ujumbe unaosema kwamba endapo watapigwa na polisi Septemba Mosi, basi viongozi wa Jeshi la Polisi wawaondoe askari wanaoishi uraiani na kuwarudisha kambini la sivyo watawashambulia:

Natoa onyo kali kwamba watu hao waache tabia hiyo…; tutawafuatilia kwa karibu kila andiko na tamko lenye mlengo wa kushabikia au kuhamasisha uhalifu aina yeyote kupitia mtandao ya kijamii. Wote walioandika au kusema kwa leno la kushabikia uhalifu huo tutawakamata ili sheria ichukue mkondo wake,”alisema Mssanzya.

MIKUTANO

Akitangaza kupiga marufuku mikutano ya ndani na kiutawala kwa vyama vya siasa, Mssanzya alisema polisi imebaini mikutano mingi inayoitishwa ina nia ya kuhamasisha vurugu jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

“Jeshi la Polisi halijazuia mikutano ya ndani, lakini katika kufuatilia suala hilo mikutano hiyo imekuwa ikitumika na watu kugawana vifaa vya kazi na kuchochea wananchi kufanya mapambano, hivyo tunapiga marufuku mikutano yoyote ya ndani, hata kama ni ya harusi,” alisema.

SEPTEMBA MOSI/ MAZOEZI

Akijibu swali kuhusu askari kufanya mazoezi ya kijeshi hadharani kamishna Mssanzya alisema: “Ndiyo, mazoezi hayo yanafanywa kwa ajili kulinda usalama wa nchi na moja ya mambo hayo ni Septemba Mosi, nguvu zitatumika na zitaongezeka kwa mujibu wa sheria.”

SHUHUDA

Mmoja wa mashuhuda wa aliyekuwa eneo hilo wakati tukio hilo lilipofanyika, Rashid Katimba aliliambia gazeti hili kwamba mauaji hayo yalitokea wakati wakati yeye akinunu matunda.

“Ndipo walipotokea hao majambazi wakiwa na silaha na kuanza kuwashambulia polisi. Kwa hali ilivyokuwa, nilijikuta nimejitumbukiza kwenye mtaro pamoja na mantunda yangu ili kujificha,” alisema Katimba.

Aliongeza: “Kwa kweli wale polisi wameuawa kinyama na inavyoonyesha majambazi husika walikuwepo maeneo hayo ya Mbande Mwisho kwa muda mre wakitafuta nafasi ya kuvamia.”

Alisimulia kwamba aliona majambazi watano, wote walikuwa na pikipiki aina ya boxer na walipomaliza kutekeleza mauaji hayo walitokomea kuelekea maeneo ya Mvunde kupitia Kisimba kuelekea njia ya Chanika.

“Mbande Mwisho hali si nzuri kabisa hali niliyoshuhudia si ya kawaida, kwa jumla hali inatisha,” alisema.

MCHAMBUZI

Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya kijeshi wanalihusisha tukio hilo na watu waliopitia mafunzo ya kijeshi wakieleza kuwa katika hali ya kawaida, mtu anayeweza kulenga risasi usoni au kichwani kama majambazi wa Mbande.

“Lile si tukio la kawaida, hata waliotekeleza lazima watakuwa wamepata mafunzo ya kijeshi tofauti nay ale ya polisi. Hilo naliamini kwani kuna watu wengi waliopata mafunzo ya kijeshi hata nje ya nchi ambao waliacha kazi hiyo na sasa haijulikani wanafanya kazi gani au walipo,” alisema mmoja wa wataalamu wa kijeshi aliyeomba kuhifadhiwa jina lake.

Alisema ipo hatari kwa watu hao kutumia vibaya mafunzo waliyopata wakiwa uraiani kama hakuna ufuatiliaji wa vyombo vya usalama, akiongeza kuwa matukio kama hayo yanaweza kutekelezwa pia na askari walio kazini iwapo hawatapata uangalizi wa kutosha ikiwapo stahiki zao kwa wakati kwani hawafanyi biashara.

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo