Sumaye alia na CCM


*Asema kumpora shamba ni njama na hila za kumdhoofisha
*Aapa kutorudi CCM na badala yake atahakikisha inang’oka

Salum Maige, Geita

Frederick Sumaye
WAZIRI Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, amesema uamuzi wa Serikali kumnyang’anya mali zake likiwamo shamba la Mabwepande, Dar es Salaam ni njama na hila za CCM kumdhoofisha kisiasa baada ya kuhamia Chadema.

Amesema Oktoba mwaka jana, Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, chini ya Waziri William Lukuvi ilimnyang’anya shamba kwa madai ya kulimiliki muda mrefu bila kuliendeleza.

Akizungumza juzi kwenye kongamano lililoandaliwa na Baraza la Vijana wa Chadema (BAVICHA), mkoa wa Geita kujadili hali ya demokrasia nchini, Sumaye alisema hata wakimnyang’anya mali wasitarajie kuwa atafilisika na kamwe hatarudi CCM.

Sumaye aliyekuwa mgeni rasmi wa kongamano hilo, alisema licha ya kunyang’anywa shamba hilo, ataendelea kuishi na maisha yake hayatabadilika na akaahidi kupambana usiku na mchana kuhakikisha CCM inaondoka madarakani.

“Mimi walininyang’anya shamba langu, nikawaambia nyang’anyeni, mimi ndiyo sasa naingia kwenye mapambano sawasawa,” alisema Sumaye na kuongeza:

“Wako marafiki zangu kule CCM wakahoji kwa nini nisirudi CCM badala ya kuteseka kiasi hicho. Na mimi jibu nililowaambia ni moja tu, nimetoka CCM kazi yangu iliyobaki ni kuiondoa CCM madarakani na si kurudi CCM.”

Alifafanua kuwa mateso wanayopata wananchi ndiyo wanayopata viongozi wa juu wa Chadema ambao baadhi yao wameanza kuteswa kwa kunyang’anywa mali zao akiwamo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliyenyang’anywa nyumba anayoimiliki kwa asilimia 75.

Alisema licha ya Mbowe kunyang’anywa nyumba hiyo ambayo hakuitaja, alisema Serikali ina mpango wa kumpora pia shamba analolima kilimo cha kisasa.

Akizungumzia hali ya kisiasa nchini, Sumaye ambaye ni mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Chadema Taifa, alisema uamuzi wa Rais John Magufuli kuzuia vyama vya upinzani kufanya mikutano kwa wananchi, ni kinyume na Katiba ya Tanzania na haijawahi kutokea hali hiyo tangu vyama vingi vilipoanzishwa.

Alisema kwa katazo hilo, hakuna mtu atakayeanzisha chama cha siasa kwani kuanzisha chama lazima ifanyike mikutano ya hadhara kutafuta wananchi, lakini kwa hali hiyo hakutakuwa na usajili wa vyama.

“Hata Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mtungi anajua hilo kwamba demokrasia imekandamizwa. Nasi hatuogopi kumwambia Rais ambayo si ya kufanya kwani hana ruhusa ya kuvunja Katiba kwani aliapa kuilinda na kuitetea,” alisema Sumaye.

Aidha, alisema kama hali itaendelea hivyo pamoja na hali ngumu ya maisha ya Watanzania njia itakuwa nyeupe ya Chadema kuingia madarakani, na hivyo aliwataka vijana kuwa mstari wa mbele kuipinga Serikali na kutetea demokrasia.

Baadhi ya wananchi walisema hali ya maisha ni ngumu na imefikia hatua ya wanaume kutelekeza familia zao kwa kushindwa kuzihudumia.

Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake (BAWACHA) jimbo la Geita, Mary Paschal alisema kuna familia zimetelekezwa na wanaume kwa sababu ya maisha magumu.

“Akina mama wengi tumekuwa wahanga wa maisha magumu, wanawake tunahangaika sana kwani akina mama tunapoomba matumizi wanaume wanachukua suruali na kuondoka bila kuaga,” alisema Mary.

Awali Mwenyekiti wa BAVICHA Mkoa wa Geita, Neema Chozaile alisema lengo la kongamano hilo ni kujadili hali ya demokrasia nchini ambapo alisema demokrasia inataka kupotezwa kwa kunyimwa uhuru wa habari, kujieleza na kutoa maoni.

Alisema Serikali iliyopo ni ya kwanza kujitokeza kubinya demokrasia nchini kwa kunyima uhuru hasa wa vyama vya siasa kujieleza kwa wananchi.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo