CUF sasa yamtaka Maalim Seif afunguke


Celina Mathew

Maalim Seif Sharif Hamadi
CHAMA cha Wananchi (CUF) kimemtaka Maalim Seif Sharif Hamad kueleza ukweli ili jamii ipate kuelewa kinachoendelea ndani ya chama hicho hasa kuhusu mambo muhimu.

Hayo ni pamoja na suala la nafasi yake ya ukatibu mkuu kukaimiwa, Bodi ya Wadhamini na kesi nne mahakamani, ambazo Seif na wenzake walifungua.

Taarifa iliyotolewa na Kaimu Katibu Mkuu wa CUF, Magdalena Sakaya jana ilieleza kwamba anachofanya Maalim Seif na wenzake ni kuwatoa wana CUF kwenye hoja za kikatiba za kushughulikia mgogoro wa uongozi ndani ya chama hicho.

Kuhusu suala la kukaimiwa kwa nafasi ya Katibu Mkuu, Sakaya alisema hilo ni  suala la kikatiba na si utashi wake au wafuasi wake.

"Tumeeleza na kunukuu ibara ya 93 kifungu cha 2 mara kadhaa. Kifungu hiki kinampa madaraka Naibu Katibu Mkuu anayetoka upande wa pili wa Muungano tofauti na anaotoka Katibu Mkuu, kukaimu nafasi na kutekeleza majukumu ya Katibu Mkuu mpaka pale Katibu Mkuu atakapokuwa tayari kutekeleza majukumu yake," ilisema taarifa hiyo ikimnukuu Sakaya.

Alisema anachopaswa kufanya Maalim Seif ni kusema kifungu hicho hakipo au hakisemi hivyo, ili jamii ipate kuelewa na si kubadilisha maneno.

“Ni kweli CUF tumeandika barua kumjulisha Msajili wa Vyama vya Siasa kuhusu suala hilo naye amejibu akikiri kupokea barua na ameridhia kwa mujibu wa Katiba yetu,” alisema.

Alisema Profesa Lipumba na Maalim Seif hakuna kati yao mwenye uwezo wa kumsimamisha mwenziwe au kuteua mtu wa kukaimu nafasi ya mwenziwe na kwamba suala la Maalim Seif kuomba kusajili Bodi mpya, na nakala ya maombi hayo kuyawasilisha Ofisi ya Msajili ni kichekesho kama si kujichanganya.

"Maalim Seif na genge lake wamefungua kesi Mahakama Kuu ya kutotambua msimamo na ushauri wa Msajili kuhusu uliokuwa mgogoro wa uongozi ndani ya CUF na inaitaka Mahakama Kuu itamke kuwa Msajili wa Vyama hana haki ya kuangalia mambo ya ndani ya CUF.

“Swali kwa Maalim Seif na genge lake,  je wanapopeleka nakala ya maombi ya kusajiliwa Bodi yao Ofisi ya Msajili huko si kuingilia mambo ya ndani ya vikao vya chama ? Au ndio kusema kwamba sasa Seif na genge lake wameamua kumtambua Msajili kupitia nyuma ya pazia?”

Aliongeza kuwa lingekuwa jambo jema kama Maalim Seif sasa angekiri wazi kwamba chama hicho kikatiba hakina Bodi halali kama ambavyo Msajili alisema kwamba Bodi ya Wadhamini ya CUF ni mfu na haipo kisheria, ndiyo maana sasa anahangaika kusajili Bodi mpya.

Alihoji kama hivyo ndivyo, je Maalim Seif anaweza kuieleza jamii na wana CUF kwa ujumla kuwa zile kesi nne mahakamani zilifunguliwa na Bodi ipi ikiwa hivi sasa yeye anaomba kusajili Bodi mpya? Au ndiyo kusema ameamua kufuta kesi zote kimyakimya?

Aliongeza kuwa ni vema akasema wazi ikiwa maombi yake ya kufungua Bodi mpya yatakubalika na kueleza ni ipi sasa itasimamia kesi mahakamani.  

"Maalim Seif hajui atendalo kwa sasa, ni vyema amwache Kaimu Katibu Mkuu Sakaya na Kamati mpya ya Utendaji wasimamie shughuli za chama ikiwamo ya kuwafanyia kampeni na kuwaombea kura wagombea wetu wa Bunge la Afrika Mashariki  na Kaimu Katibu Mkuu yuko Dodoma akifanya kampeni kwa wagombea wetu Habib Mnyaa, Thomas Malima na Sonia Magogo,” alisisitiza.

Aliwajulisha wana CUF kokote waliko na Watanzania kwa jumla yao kuwa chama hicho kiko katika mikono salama ya viongozi wanaojitambua ambao hawaendeshwi kwa fedha za kifisadi, bali wanaendesha chama kwa mujibu wa Katiba yake ya mwaka 1992 toleo la 2014.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo