Tembo waongeza tatizo la chakula


Costantine Mathias, Itilima

WAKATI baadhi ya maeneo ya nchi yakikabiliwa na upungufu wa chakula kutokana na ukame, kata za Nkuyu, Migato na Mwaswale wilayani hapa zimevamiwa na tembo na kuharibu mazao yao.

Wakizungumza na waandishi wa habari jana, baadhi ya wananchi walieleza kuwa ekari zaidi ya 130 za mazao ya chakula zimeharibiwa na tembo hao.

‘’Tembo zaidi ya 50 jana (juzi) waliingia mashambani na kula mahindi, mtama na kuharibu pamba, tulijaribu kuwafukuza kwa kutumia njia za kienyeji lakini walionekana kuwa wakali hadi saa 8 usiku tukaamua kuwaacha na kwenda kulala,’’ alisema Nilla Derefa, mkazi wa Nyantugutu.

Nilla alisema wanyama hao waliwahi kufika katika maeneo hayo lakini wakawafukuza kwa kupiga ngozi ya ng’ombe na kengele, lakini juzi walikuwa wakali kupita kiasi.

Shigulu Mlasi, ambaye pia ni mkazi wa eneo hilo, alisema tatizo la tembo limewaathiri kwani walijitahidi kulima mapema, lakini tembo wamekula mazao yao na sasa hawana matumaini ya kupata chochote mashambani humo.

‘’Tembo wana walinzi wao, iweje wavamie makazi ya watu? Sheria ya kulinda tembo na wanyamapori iangaliwe upya, kwa kuwa tembo akimwathiri binadamu hakuna hatua zinazochukuliwa haraka, lakini binadamu akimwathiri tembo atatafutwa hata kama yuko nje ya nchi,’’ alisema Mlasi.

Diwani wa Nkuyu, Ndulu Mtegwa alisema ofisi ya kilimo ya wilaya imeshapewa taarifa ingawa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa kuwanusuru wananchi hao.

Alisema tembo hao wamekuwa tishio kwa maisha ya wananchi na mazao yao huku akiitaka Serikali kulipatia ufumbuzi suala hilo kwani maeneo hayo yamekuwa kama makazi ya tembo.

Alitaja kata jirani na yake ambazo ni Migato na Mwaswale kuwa nazo zimeathiriwa na wanyama hao na hadi sasa wananchi hawana imani na viongozi wao, ambao wamekuwa wakitoa taarifa serikalini bila kuona hatua zozote za utekelezaji.

‘’Vijiji vilivyoathiriwa na tembo hao ni Lung’wa, Pijulu, Nyantugutu, Longalombogo, Shishani, Ng’walali na Nding’ho. Tunaiomba Serikali kupitia wataalamu wa wanyamapori, waje kuwanusuru wananchi hawa,’’ alisema Diwani huyo.

Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Benson Kilangi alisema ofisi yake haijapata taarifa ya tembo hao kuharibu mazao ya wananchi.

‘’Hizo taarifa hazijafika ofisini kwangu, lakini tumekuwa bega kwa bega na wananchi wanapopatwa na matatizo kama hayo kwani huwa tunahakiki uharibifu wao kupitia viongozi wao, ili kutoa tathimini ya uharibifu,’’ alisema Kilangi.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo