JPM atema cheche Sheria


*Ashangaa Mwanasheria Mkuu, DPP kuvutana
*Aitaka Mahakama kusimamia kesi kwa weledi

Suleiman Msuya

Rais John Magufuli
“LEO nawapa makavumakavu.” Hiyon ni kauli ya Rais John Magufuli alipozungumza jana na familia ya wanasheria katika maadhimisho ya Siku ya Sheria yaliyofanyika Dar es Salaam.

Rais aliamua kufunguka akitumia kauli yake ya Msema Kweli ni Mpenzi wa Mungu akizungumzia uozo ndani ya Mhimili wa Mahakama, lakini pia katika Wizara ya Sheria na Katiba.

Pamoja na mambo mengine, Rais Magufuli aliweka bayana mgogoro ulio katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Biswalo Mganga bila kupatiwa ufumbuzi.

Aidha, aliitaka Mahakama kufanya kazi kwa weledi bila kupendelea, kwani kufanya hivyo kunasababisha wananchi kukosa imani na chombo hicho akitolea mfano mahakimu 28 waliokuwa wakituhumiwa kuachwa huru na sakata la Escrow.

Alisema yapo mambo mengi ambayo wanayasikia na amekuwa akiyanyamazia, lakini inafikia mahali inamlazimu aseme kutokana na ‘madudu’ yanayofanyika.

Rais alisema inashangaza viongozi hao ambao kiasili wanatoka mkoa mmoja (Mara) kila siku wanalumbana jambo ambalo linasikitisha na kushangaza.

“Tunayasikia, ni mengi katika ofisi ya AG na DPP, ofisi hizi zinagombana zenyewe kwa zenyewe, nani hajui nawaulizeni nani hajui hapa, nasema uongo jamani, Waziri unafahamu kwamba kuna mgogoro katika ofisi hizo mbili na kwamba wanatoka mkoa mmoja na inawezekana wilaya moja,” alisema.

Magufuli alisema waziri, DPP na AG wanapaswa kukutana na kupata mwafaka ili mambo yaweze kwenda na kwamba wote ni wateule wa Rais, hivyo kama ni masuala la kasma wazungumze na atangaalia njia ya kutatua, kwani utaratibu unamruhusu.

Alisema mgogoro unaweza kuwa sababu ya Serikali kushindwa kila kesi ambayo inafunguliwa, kwa sababu wahusika wa kutetea hawako pamoja, hali inayosababisha majaji kuahirisha kesi kila siku kwa kuamini kuwa wahusika watatambua tatizo.

Aidha, alisema eneo lingine lenye changamoto ni Jeshi la Polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kwani hawafanyi upelelezi huku wakiwa na ushahidi wa jambo husika.

“IGP upo hapa, leo nawapa tu zote kavukavu haiwezeni umemshika mtu na pembe za ndovu, dawa za kulevya waziwazi halafu unasema upelelezi haujakamilika unataka ukamilikeje?” Alihoji.

Rais alisema kudai upelelezi unafanyika kumesababisha wakati mwingine ushahidi kupotea na mhusika kutoingizwa hatiani.

Alisema katika mazingira hayo ya vyombo husika kuchelewesha upelelezi inafikia mahali dawa za kulevya kubadilishwa na kuwa mihogo (unga) kutoka Sumbawanga, hivyo Mkemia kukosa ushahidi.

TLS

Akizungumzia Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) alikitaka kiache kuwa na mrengo wa kisiasa ili kusaidia nchi na kuweka bayana kuwa hatateua wakili wa chama hicho kama kitakuwa na mrengo huo.

Alisema ana taarifa za baadhi ya wanachama kushabikia siasa na kuwa wapo wanaotarajia kugombea uongozi.

“TLS imekuwa kama chama cha siasa na hata hivi sasa kuna kampeni za watu kutoka chama fulani kutaka kukurithi wewe, naamini kuwa mnatakiwa kuangalia maslahi ya nchi kwa kuwa watu wa kati kwa maendeleo ya nchi,” alisema.

Msajili

Kwa upande mwingine alisema inasikitisha kuona Mahakama inafanya ubaguzi katika usajili wa kesi akiweka bayana kuwa kuna mbinu zinatumika kwenye usajili.

Bajeti

Kuhusu bajeti na maslahi ya wafanyakazi wa Mahakama, alisema ataangalia jinsi ya kufanya huku akiitaka Mahakama kuwa sehemu ya kuchangia pato la Taifa.

Alisema inasikitisha watu wanakwepa kodi na hata Mahakama inapohukumu utekelezaji au ukaziaji hukumu linakuwa tatizo.

“Serikali imeshinda kesi za kodi tangu mwaka 2001 zinazofikia Sh trilioni 7.5 zimepakiwa pamoja na hukumu za kwanza kutolewa na tukashinda, najua mnahitaji mshahara mkubwa na marupurupu, ila isiwe sababu ya kutetea wakwepa kodi,” alisema.

Alisema kuna utaratibu wa kesi kuwekewa pingamizi huku kesi kama hizo za kodi katika nchi nyingine, zinasikilizwa na kutolewa uamuzi haraka bila kuangalia mhusika ni nani.

Alisema wapo majaji ambao kokote wanakopita wanakubalika kutokana na kazi zao zilizotukuka ila wapo ambao kila kesi wakipelekewa wanashindwa, hao hawafai na wanapaswa kuchunguzwa.

Alisema inashangaza Mahakama kutoa hukumu zinazofanana kwa watuhumiwa wa sekta hiyo, na kutolea mfano mahakimu 28 walioshitakiwa kwa rushwa lakini wote wakashinda.

Halikadhalika suala la Escrow ambalo lilihusisha majaji lakini hakuna hatua iliyochukuliwa, jambo ambalo linajenga imani mbaya kwa wananchi.

Rais alisema katika mazingira yanayoibua maswali, mwaka jana majaji 80 waliomba likizo, licha ya Serikali kutotoa fedha za likizo kwa majaji 74, wapo ambao waliokwenda nje ya nchi na kukaa mwezi mmoja hivyo kuibua maswali ya nani aliwalipia kwenda nje.



Kaimu Jaji Mkuu

Awali akizungumza katika sherehe hizo, Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma alisema mahakama imejipangia kutekeleza mkakati wa miaka mitano wenye lengo la kubadilisha muhimili huo na kufanikisha mpango wa Taifa wa miaka mitano

Alisema kuna maeneo matatu ya mpango ambayo ni utawala bora, uwajibikaji na usimamizi wa rasilimali, upatikanaji haki kwa wakati na uimarishaji imani ya wananchi na ushirikishwaji wadau kwenye shughuli za kimahakama.

Alisema moja mikakati yao ni kuona muhimili huo unakuwa chachu ya kukuza uchumi ikiwa ni kuungana na Benki ya Dunia ambayo inazitaka mahakama kuwa hivyo.

 “Napenda kuwapongeza wananchi na wadau wote ambao kwa pamoja tumekuwa tukishirikiana kuhakikisha kuwa changamoto zilizo katika mahakama zinatatuliwa,” alisema.

Mwenyekiti wa TLS, John Seka alisema wamejipanga kushirikiana na Serikali kuhakikisha dhana ya uchumi wa nchi inatekelezeka.

Aidha, Seka alimwomba Rais kumthibitisha Profesa Juma kuwa Jaji Mkuu kwa alichodai kuwa na sifa zote ambazo ni weledi na uwezo.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo