…’Amwaga mboga’ mbele ya Magufuli


Suleiman Msuya

Swabaha Mohamed mbele ya JPM
MWANAMKE mkazi wa Tanga, Swabaha Mohamed, amezusha taharuki kwenye sherehe za Siku ya Sheria kwa ‘kufunguka’ mbele ya Rais John Magufuli akidai kunyimwa haki na vyombo vya kutoa haki nchini kuhusu mirathi yake.

Mwanamke huyo aliibuka muda mchache baada ya Rais Magufuli ‘kuwatolea uvivu’ baadhi ya viongozi wa vyombo hivyo; Polisi, Mahakama, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka  (DPP) na ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kuwa zinashindwa kufanya kazi kwa pamoja.

Swabaha ambaye alikaa viti vya nyuma akionekana mtulivu na kufuatilia hotuba ya Rais, mwishowe alisimama akiwa na bango la kitambaa lenye maandishi yakisema vyombo hivyo vinamnyima haki.

Kitendo cha Swabaha kilishitua watu wakiwamo wa Usalama hasa  alipoelekea mbele ili Rais asome ujumbe wake, ndipo mmoja wa watu wa Usalama alipomfuata na kumrejesha eneo lake.

Hata hivyo mwanamke huyo alionesha kupinga ndipo ofisa mwingine akaongeza nguvu na kumrejesha kwenye kiti chake huku maofisa wengine wawili wakiongezeka na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro kuungana nao kumdhibiti.

Baada ya Rais kuona hali hiyo, aliamuru mwanamke huyo aachwe na apewe nafasi ya kueleza anachotaka akiwa karibu naye, maofisa hao walimruhusu huku wakimtaka aende bila nyaraka zake.

Kitendo cha kumtaka aache nyaraka kilimfanya apayuke na Rais akaagiza nyaraka hizo apewe na baada ya kupewa akaelezea   kinachomsibu.

Swabaha alimweleza Rais kuwa kwa takribani miaka minne anafuatilia haki yake ya mirathi ila kuna watendaji wa Serikali wanakwamisha kwa makusudi.

Alisema baada ya mumewe kufariki dunia mwaka 2012 walijitokeza watu wakiwamo wanawake aliozaa nao, mmoja ni mpangaji wake aliyemtaja kwa jina la Alfred Akaro na mwanawe wa nje, wakishirikiana na wakili wa Serikali aliyemtaja kwa jina moja la Rebeca kutaka kumdhulumu haki yake ya mirathi.

Alisema mumewe alioa wake wawili ambao ndio wanastahili kupata mirathi kwa mujibu wa wosia alioacha, lakini katika mazingira ya kutatanisha, kundi hilo lilitengeneza nyaraka bandia ili kuwadhulumu.

Mjane huyo alisema amefikisha malalamiko yake kwenye vyombo  vya ngazi ya juu huku akikumbana na vikwazo katika baadhi ya ofisi.

“Nimehangaika sana kuhusu hili suala, ila kuna watumishi wa Serikali wanatumia kila mbinu kunidhulumu wakishirikiana na kundi la watu, hata Rais nilimtumia ujumbe akamtumia IGP,” alisema.

Swabaha alisema amepigania haki hiyo kwa muda mrefu hivyo kwa sasa anachotaka ni haki yake au afungwe, kwani anapokea vitisho kutoka kundi hilo kila kukicha na ujumbe ambao anatumiwa amekuwa akimtumia IGP.

IGP Ernest Mangu alikiri kupokea malalamiko hayo na kuwa kuna changamoto kidogo kwa kinachooneka kuwa ni suala la kifamilia na alimwelekeza Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) Boaz alifanyie kazi katika kipengele cha jinai.

Katika kuhitimisha hilo, Rais Magufuli aliwaagiza AG, DPP, IGP na Mahakama kupitia kwa Jaji Kiongozi, Ferdinand Wambali kuhamishia kesi hiyo Mahakama ya juu ili uamuzi ufanyike.

Aidha, Rais Magufuli alitoa agizo kwa Polisi kumlinda mwanamke huyo ili asije kudhuriwa na wabaya wake.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo