Tume yaonya kampeni zisizo za kistaarabu


Mwandishi Wetu 

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetaka wagombea na vyama vya siasa vinavyoendelea na kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge na udiwani kufanya hivyo kistaarabu kwa kuzingatia Maadili ya Uchaguzi ya mwaka 2015.

NEC imeonya dhidi ya chama au mgombea atakayekiuka maadili hayo kwamba atachukuliwa hatua bila kusita.

Makamu Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mkuu mstaafu wa Zanzibar, Hamid Hamid ametioa onyo hilo, siku chache kabla ya uchaguzi huo Januari 22, baada ya baadhi ya vyama na wagombea kukiuka maadili na taratibu za kampeni kwa kutoa matamko yaliyo nje ya sera za vyama vyao.

Alisema kipengele cha 2.1 (m) cha Maadili ya Uchaguzi kinaeleza Wajibu wa Vyama vya Siasa na Wagombea katika kuendesha shughuli za siasa wakati wa kampeni, kikivitaka vyama vya siasa, wagombea na wafuasi wao, kukampeni kwa kuzingatia misingi ya kutangaza sera zisizo za chuki, mifarakano wala mgawanyiko katika jamii.

“Katika kampeni zinazoendelea, baadhi ya vyama vya siasa vimeanza kukiuka taratibu za kampeni na maadili na kutumia fursa ya kampeni vibaya, vinawasema viongozi wa kitaifa, kutoa matamko ambayo kihalisia si ya kunadi mgombea na kufanya kampeni zisizo za kistaarabu,” alionya Jaji Hamid.

Alisema vyama au wagombea watakaoendelea kukiuka Maadili ya Uchaguzi katika mikutano ya kampeni inayoendelea katika maeneo mbalimbali ya Tanzania na Jimbo la Dimani, Zanzibar watachukuliwa hatua.

Jaji Hamid alieleza kuwa kipengele cha 5.3 cha Maadili ya Uchaguzi kinaeleza wazi kuwa chama au mgombea atakayekiuka maadili ya uchaguzi katika jimbo au kata yenye uchaguzi mdogo, atafikishwa katika Kamati ya Maadili ya ngazi husika na kuchukuliwa hatua stahiki.

Aidha, kipengele cha 5.10 cha Maadili ya Uchaguzi yaliyokubaliwa na vyama vyote vya siasa, kinafafanua kuwa kamati za maadili ya uchaguzi Taifa, Jimbo na Kata katika kushughulikia malalamiko na kutoa adhabu, zinaweza kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kukitaka chama au mgombea kusahihisha kosa au makosa au kuomba msamaha hadharani.

Hatua nyingine ni kukisimamisha chama au mgombea kuendelea kufanya kampeni za uchaguzi, kutoza faini, kutangaza jina la chama au mgombea aliyekiuka maadili kwa kueleza kosa au makosa yake kupitia redio, televisheni, magazeti na njia nyingine za mawasiliano.


Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo