MSD: Upatikanaji dawa utaongezeka


Peter Akaro

BOHARI ya Dawa (MSD) imesema upatikanaji wa dawa nchini unatarajiwa kuwa kati ya asilimia 86 hadi 90 kwa Januari hadi Machi.

Akizungumza jana Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu alisema baada ya kuwasili kwa awamu mbili za dawa kutakamilisha aina 100 za dawa kati ya 135 muhimu.

Bwanakunu alisema Serikali ilifanya uchunguzi kwenye kitengo hicho ili kuboresha huduma na kubaini mambo kadhaa ambayo ndiyo yamefanyiwa kazi.

Mambo hayo ni ufinyu wa bajeti, kuangalia kama sheria iliyoanzisha MSD mwaka 1993 inasadia utendaji na shughuli, upanuzi wa wigo wa mikataba, kuboresha taratibu za malipo kwa wazabuni na kuboresha njia za kupata fedha tofauti na zilizopo sasa.

Alisema MSD imeachana na mpango wa kukodi maghala ya kuhifadhi dawa ambayo yalikuwa yanawagharimu Sh bilioni nne, ila sasa wameanza ujenzi wa ghala katika kiwanja cha Luguruni, Ubungo kwa kanda ya Dar es Salaam.

Alisema pia MSD imeanza utaratibu wa kununua dawa na vifaatiba moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji, utaratibu unaopunguza gharama za ununuzi wa dawa na vifaatiba kutoka kwa wafanyabiashara.

“Hadi sasa MSD imetoa mikataba 58 ya ununuzi wa dawa muhimu, na imetangaza zabuni ambayo itafunguliwa Januari 28, tunatafuta walizashaji 76 wa dawa na 79 wa vifaa,” alisema.

Alisema MSD inaendelea na huduma maalumu kwa wateja wake wakubwa ili kuwawezesha kupata huduma kwa haraka zaidi, wateja hao ni hospitali za Muhimbili, Kibong’oto, Mirembe, Amana, Temeke, Mwananyamala na KCMC.

Pia kuna Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya, Benjamin Mkapa ya Dodoma na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete.

Kwa sasa MSD ipo katika mchakato wa kuanzisha viwanda vya kuzalisha dawa na vifaatiba kupitia mpango wa ushirikishaji sekta binafsi.

Aliongeza kuwa mwaka jana MSD ilifungua maduka sehemu mbali mbali nchini kwa lengo la kuwezesha hospitali.

Maduka ambayo hadi sasa yamefunguliwa ni la Muhimbi, Mount Meru, Arusha; Sekou Toure, Mwanza; Mbeya; Chato, Geita na Rungwe, Lindi.

“Kwa sasa tuko mbioni kufungua duka la Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda, Katavi,” alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo