Salha Mohamed
WANAHABARI wameaswa kutoogopa na
kukatishwa tamaa na vifungu vichache vya Sheria ya Habari iliyosainiwa na Rais
John Magufuli hivi karibuni, badala yake wanatakiwa kuisoma sheria hiyo na
kuielewa.
Hayo yalibainishwa Dar es Salaam jana na
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Theophil Makunga, wakati wa mkutano wa
siku mbili uliowakutanisha wahariri wa vyombo vya habari hapa nchini.
Mkutano huo wa wahariri ulioanza jana na
kumalizika leo, umelenga kupitia sheria ya huduma za vyombo vya habari na
kujadili mpango mkakati wa TEF, wa kuendeleza tasnia ya habari, huku wakipata
uzoefu kutoka nchi za Kenya na Afrika Kusini.
Kupitia mkutano huo, Makunga alisema
hakuna haja ya wanahabari kuogopa au kuwa na wasiwasi kuhusu sheria hiyo
iliyosainiwa hivi karibuni na Rais John Magufuli.
“Kama tuliweza kuishi na sheria ya
magazeti ya mwaka 1976 basi tunaweza hata chini ya hii sheria mpya….kwa sababu
hii sheria ni afadhali kuliko ile ya mwaka 1976.
“Imepunguza vitu vingi sana ambavyo
vilikuwa amepewa mtu mmoja na badala yake kuhamishiwa kwa bodi, hivyo kuna vitu
ambavyo ni vizuri katika hii sheria kuliko ile ya mwaka 1976,”alisema.
Makunga alifafanua kuwa awali katika muswada
wa habari, suala la elimu lilionesha kuwa ni lazima mwandishi afike ngazi ya Stashahada huku
sheria ikiwa haijaonesha hivyo.
Makunga aliongeza kuwa wanasubiri kanuni
za sheria hizo zitasemaje huku akibainisha kuwa angependa kipengele cha elimu kiwe
na ngazi ya mwandishi gani anafanya nini kwa wakati gani.
“Hakuhitaji stashahada kwenda kuandika habari
pale kambi ya fisi. Ila kwa mhariri suala la stashahada ni jambo zuri, kwani
itamsaidia kuwa na upeo mkubwa wa kutoa uamuzi, mwandishi si lazima,”alisema.
Makunga alisema katika sheria hiyo kuna
vipengele vichache hatarishi kwa mwandishi, huku akibainisha kuwa vinaweza
kufanyiwa marekebisho ya vifungu kama serikali itakubali.
Aliongeza kuwa tayari sheria ya habari imesainiwa
kinachotakiwa ni kuona namna ya kuendesha tasnia ya habari na kuimarika chini
ya sheria hiyo bila kuathiri uendelezaji wa taaluma ya waandishi wa habari.
Mwanahabari mpekuzi wa nchini Kenya,
Mohamed Ali alisema waandishi wa habari wa Tanzania ni waoga zaidi duniani.
“Tanzania ipo ambapo Kenya ilikuwa miaka
ya 1980, ambapo hakukuwa na uhuru wa habari na thulma ya kila aina ikiwemo
kuuwa,”alisema.
Alisesma nchini kwao walipinga na kutaka
kuwa na uhuru wa kuzungumza na walifaulu ingawa kulikuwa na changamoto ndogo
ndogo.
“Ukiangalia Tanzania wamekubali kuwa
waoga kila mtu atasema hakuna shida, lakini hakuna mtu anayeweza kusimama na
kusema anaweza kukomboa kwa niaba ya taifa zima,”alisema.
Aliongeza kuwa Watanzania wanahitaji
kukataa sheria hizo ambazo zitagandamiza haki ya kila Mtanzania kama ambavyo
wao walikataa na kuzikataa sheria hizo.
“Ni jukumu lenu Watanzania msimame hizi
sheria si za wanahabari bali ni za Tanzania, maana ukimzima mwanahabari umezima
Tanzania,” alisema.
0 comments:
Post a Comment