Fidelis Butahe na Suleiman Msuya
Profesa Ibrahim Lipumba |
WAKATI Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec)
ikitangaza ratiba ya uchukuaji fomu kujaza nafasi ya mbunge na madiwani zilizo
wazi, vyama vinavyounda Ukawa viko mtegoni kutokana na mgogoro uliokigawa Chama
cha Wananchi (CUF).
Jana baadhi ya viongozi wa vyama
vinavyounda Ukawa vya Chadema, NLD na NCCR-Mageuzi viliiambia JAMBO LEO kuwa vitashirikiana
katika uchaguzi huo mdogo na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, na
si Mwenyekiti wa Chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba.
Wakati viongozi hao wakieleza hayo, Naibu
Katibu Mkuu wa CUF -Bara, Magdalena Sakaya
anayemuunga mkono Profesa Lipumba, alisema chama hicho kitafanya vikao
kwa mujibu wa Katiba ili kupata wagombea
kwenye uchaguzi huo, kauli ambayo ilipingwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi
ya Chama hicho, Julius Mtatiro.
Katika uchaguzi mkuu mwaka jana, vyama
hivyo vilishirikiana kusimamisha mgombea mmoja kwenye baadhi ya majimbo na kata
huku kwa pamoja vikimpitisha na kumuunga mkono mgombea urais wa Chadema, Edward
Lowassa.
Mgogoro ndani ya CUF ulianza baada ya
Profesa Lipumba kuandika barua ya kutaka kurejea kwenye uenyekiti, ikiwa
imepita miezi 10 baada ya kujiuzulu, jambo ambalo lilizua mgogoro mkubwa, ikiwa
ni pamoja na kuvunjika kwa Mkutano Mkuu uliompitisha Mtatiro kuwa Mwenyekiti.
Baada ya mvutano huo, Baraza Kuu la
Uongozi la Chama hicho lilimvua uanachama Profesa Lipumba na baadaye kumfukuza
uanachama, huku Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ikitoa tamko la kumtambua
kuwa mwenyekiti wa CUF.
Kwa tamko hilo la Msajili, Baraza la
Wadhamini la CUF lilifungua kesi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kupinga
kurejeshwa kwa Lipumba.
Kutokana na mvutano huo, jana baadhi ya
viongozi wa Ukawa walitoa msimamo kuhusu uchaguzi huo katika jimbo la Dimani, Zanzibar
na kwenye kata 22.
Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Danda Juju
alisema: “Chama chetu hatuamini uwepo wa Lipumba katika CUF. Kama chama,
tutaendelea na ushirikiano wa Ukawa ikiwa ni pamoja na kuamua mgombea wa chama
gani agombee kulingana na taratibu tulizojiwekea.”
Juju alisema Mtendaji Mkuu wa CUF ni
Katibu Mkuu si Mwenyekiti na katika vikao vyote vya Ukawa, wamekuwa
wakishirikiana na Maalim Seif, hivyo hakuna uwezekano wa kuungana na Lipumba.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Katibu Mkuu
wa NLD, Tozi Mtwange na kusisitiza kuwa Profesa Lipumba aliondolewa na vikao
vya CUF kwa mujibu wa Katiba, hivyo hawawezi kushirikiana naye katika uchaguzi
huo.
Mtatiro alisema: “Chama kitakutana
kupitisha wagombea. Hao wengine (wafuasi wa Profesa Lipumba) hawawezi kufanya
vikao vya uamuzi.”
Alisema vikao hivyo vitaanza muda wowote
kuanzia sasa na kusisitiza kuwa ushirikiano wa Ukawa kwenye kata na jimbo hilo
utaendelea kama ilivyokuwa kwenye Uchaguzi Mkuu, ikiwa ni baada ya viongozi
wake kukutana na kupanga wagombea wa chama gani watakaopeperusha bendera za
vyama vyao na Ukawa katika uchaguzi huo.
Kauli ya Mtatiro ilipingana na ya Sakaya
ambaye awali alilieleza gazeti hili kuwa vikao vya kupitisha wagombea wa CUF kwenye
kata hizo vitafanyika kwenye wilaya husika, kwamba kwa mgombea wa Dimani,
uamuzi utatolewa na uongozi wa chama hicho kwenye jimbo hilo.
Kwa mujibu wa ratiba ya NEC, fomu za
uteuzi kwa ajili ya uchaguzi huo zitaanza kutolewa Desemba 10 hadi 22 ukifuatiwa
na uteuzi wa wagombea Desemba 22, wakati Desemba 23 hadi Januari 21 ni muda wa
kampeni ambapo Januari 22, itakuwa siku ya kupiga kura.
NEC itaendesha uchaguzi mdogo kujaza
nafasi za wazi za udiwani kwenye kata 22 katika baadhi ya halmashauri za
Tanzania Bara zilizokuwa wazi kutokana na sababu mbalimbali.
0 comments:
Post a Comment