Nyumba 500 zabomolewa kimakosa Dar es Salaam


* Amri ya Mahakama ililenga nyumba 5 tu
* Wabomoaji wanogewa na kuvuka mpaka

Stella Kessy

UBOMOAJI nyumba 500 uliofanywa Kivule, Dar es Salaam hivi karibuni ulifanyika kimakosa kwa kuwa zilizotakiwa kubomolewa zilikuwa ni tano tu.

Kutokana na zahama hiyo, wakazi waliiovunjiwa nyumba hizo kimakosa wamepanga kwenda Mahakama Kuu kufungua kesi ya madai.

Uamuzi wa wakazi hao, unakuja siku chache baada bomobomoa hiyo, huku ikielezwa kuwa hati ya Mahakama iliyotoa idhini ya kubomoa nyumba hizo haikulenga nyumba 500.

Chanzo cha bomoabomoa hiyo ni mgogoro kati ya wananchi wa eneo ilo pamoja na Umoja wa Vijana wa Kikristo Tanzania (Uvikiuta) ambao unadai kuwa mmiliki halali wa eneo ilo.

Akizungumza kwa niaba ya wakazi hao jana, Diwani wa Kivule, Wilson Molel alisema wanakwenda mahakamani kufungua kesi hiyo ya madai, kwa kuwa nyumba zao zilibomolewa bila hatia na tano zilizopaswa kubomolewa ziko eneo tofauti na zilikokuwa nyumba hizo.

"Mahakama ya Temeke ilitoa idhini ya kuvunjwa kwa nyumba tano, lakini badala yake wakavunja nyumba 500, katika kesi ya msingi pande zote mbili hazikuwa zimesikilizwa, ila ulisikilizwa upande mmoja ambao ni walalamikaji Uvikiuta," alisema Mollel.

Tukio la kubomolewa kwa nyumba hizo, lilitokea Novemba 29, ambapo kwa mujibu wa Mollel, alipata taarifa za nyumba hizo kubomolewa saa 12 asubuhi kutoka kwa wananchi.

Alipofika eneo hilo alihoji sababu za kubomoa na kuomba kuoneshwa vibali, lakini akakamatwa na askari na kupekekwa Kituo cha Polisi Maturubai.

Alisema walipofika kituoni hapo, dalali wa Mahakama alitoa kibali kilichotolewa mwaka 2012 walichooneshwa kwa mbali na kuomba wakipige picha, lakini wakakataliwa, badala yake wakazingirwa na polisi.

Mollel alisema waliomba kujua utaratibu wa kisheria kuhusu kubomolewa kwa nyumba hizo kutoka kwa Ofisa Upelelezi wa Temeke na kujibiwa kuwa kilishatolewa.

Alisema baada ya kuhoji hayo, ndipo walipogeuziwa kesi na polisi kumpa karatasi Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara wakimtaka aandike maelezo kwa nini alihamasisha wananchi kushambulia polisi, akagoma akieleza kuwa anamsubiri mwanasheria wake.

“Viongozi hawana taarifa yoyote zaidi ya ubabe wa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma (Jordan Rugimbana), ndiye aliyefanya jambo hili, tumepiga simu kwa Mkuu wa Mkoa (Paul Makonda) haikupokewa, Kamanda Simon Sirro alisema yuko kwenye mkutano, sijui wananchi leo watalala wapi? Kama utendaji ndio huu ni kosa,” alisema Mollel.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo