* Ni Kama hatasitisha timuatimua ya wamachinga
* Ambana
Muhongo kuhusu mwekezaji wa madini
Waandishi
Wetu
RAIS John Magufuli ametishia ‘kuwatumbua’
Waziri na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Amesema ‘atawatumbua’ ikiwa watashindwa kusitisha
mchakato wa kuondoa wamachinga katika maeneo mbalimbali nchini, huku akimweka
kikaangoni Waziri wa Nishati na Madini kuhusu mwekezaji.
Kupitia taarifa yake kwa vyombo vya
habari iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, Rais Magufuli
alionya kuwa kiongozi asiye tayari kutekeleza maagizo yake, aachie ngazi.
Hata hivyo, Rais Magufuli alisema
maagizo yake hayana maana kuwa wamachinga na wachimbaji wadogo wanaruhusiwa
kuendesha shughuli zao kwa kuvunja sharia, bali wazingatie sheria na mamlaka
zisinyanyase wanyonge.
Agizo hilo limekuja siku chache baada ya
wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa manispaa za Nyamagana na Ilemela, Mwanza kuvunja
vibanda vya wafanyabiashara hao usiku wa manane na kudaiwa kuharibu mali zao.
Uvunjaji huo wa usiku wa maeneo ulilalamikiwa
na wafanyabiashara hao huku wakidai kuwa maeneo wanayopelekwa hayafai kwa
biashara na kuwa hakuna maandalizi yaliyofanyika kwa ajili ya biashara zao.
Rais Magufuli alitoa agizo hilo jana
akiwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na kubainisha kuibuka tabia ya
baadhi ya wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi, kufukuza wamachinga bila
utaratibu.
Alisema mchakato wa kuhamisha wamachinga
unatakiwa kufanyika pale ambapo mamlaka husika zimekamilisha maandalizi ya
maeneo wanayohamishiwa kwa kushirikisha wamachinga wenyewe.
“Wakati mwingine mnawapeleka maeneo ya
mbali ambayo hayafai hata kwa biashara, hili jambo si sawa hata kidogo.
"Sipendi wamachinga wafanye
biashara kwenye hifadhi za barabara, lakini hakuna sheria katika nchi hii,
inayosema mtu wa biashara ndogo ndogo au mmachinga hatakiwi kukaa katikati ya
mji, tukianza kwenda kwenye utaratibu wa namna hiyo, maana yake tunaanza
kutengeneza madaraja ya Watanzania,” alisema.
Alisema utaratibu huo utaanza kuonesha
kuwa kuna Watanzania fulani wa daraja fulani wanapaswa kukaa katikati ya mji na
Watanzania wa daraja fulani hawatakiwi kukaa katikati ya mji.
“Huo si mwelekeo wetu na wala Ilani ya
Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambayo mimi na wewe (Makamu wa Rais)
tulipita kuinadi, haisemi tutengeneze madaraja ya watu wanaostahili kukaa mjini
na wengine hawastahili kukaa mjini, sasa nimeona hili nilizungumze na nataka kulirudia
kwa mara ya mwisho," alionya Rais Magufuli.
Dk Magufuli alielekeza kuwa wamachinga
waliondolewa kwenye maeneo yao Mwanza waachwe waendelee na shughuli zao mpaka
hapo Halmashauri ya Jiji la Mwanza, itakapokamilisha maandalizi ya mahali
watakapohamishiwa na kwa kuwashirikisha wamachinga wenyewe.
"Narudia, na hii ni mara ya mwisho,
kawaambieni hata wamachinga wa Mwanza warudi kwenye maeneo yao, mpaka
watakapowatengenezea utaratibu mzuri,” alisema.
Rais alisema Kigamboni palikuwa na
wamachinga na walihama vizuri na kutengenezewa miundombinu yao katika soko lao
na sasa hivi wanafanya kazi vizuri.
Alisema mafanikio ya Kigamboni
yamechangiwa na ushirikishwaji wa viongozi wa wamachinga, lakini Mwanza imekuwa
ni amri tu na wengine wanatumia hata usemi wa ‘Hapa Kazi Tu’.
“Mimi sikusema usemi wa ‘Hapa Kazi Tu’
wa namna hiyo, nadhani mmenielewa," alisisitiza Rais Magufuli alipokuwa
akiwaekeleza Naibu Waziri wa Tamisemi, Suleiman Jaffo na Katibu Mkuu, Mussa
Iyombe.
Katika
hatua nyingine, Rais Magufuli aliagiza Wizara ya Nishati
na Madini kusitisha mara moja mchakato wa kuondoa wachimbaji wadogo kwenye kijiji
cha Nyaligongo kata ya Mwakitolyo mkoani Shinyanga.
Alitaka wachimbaji hao waachwe waendelee
na shughuli zao na kuagiza leseni ya mwekezaji ifutwe na anayedai eneo hilo ni
lake aondolewe.
“Wale waliofukuzwa Shinyanga wabaki
palepale, kama ni leseni ya huyo mwekezaji ifutwe, Makamu wa Rais fuatilia
hili, mweleze Waziri husika (Profesa Sospeter Muhiongo), waache kufukuza
wananchi hovyo hovyo, wale wanapata riziki yao, wanasomesha watoto wao lakini
wanafukuzwa tu.
“Na hizi ndizo ajira zenyewe, tulisema
tunatengeneza ajira, wewe mwekezaji ni mmoja, unakwenda kufukuza watu 5,000! Haiwezekani
na wala haingii akilini,” alisisitiza Rais Magufuli.
Rais pia alikemea vitendo vya wawekezaji
wakubwa kupewa maeneo ambayo wachimbaji wadogo wanaendesha shughuli zao, wakifanya
hivyo kwa mtindo wa kutengeneza nyaraka zinazoonesha mwekezaji husika alipewa
eneo hilo kabla ya wachimbaji wadogo na kusisitiza kuwa mchezo huo hautavumiliwa.
Simbachawene
Wakati
huo huo, Waziri wa Tamisemi, George Simbachawene
alikiri kukutana na Rais Magufuli ambako alielezwa kuwa hafurahishwi na jinsi
wakuu wa mikoa, wilaya na wenyeviti wa serikali za mitaa wanavyonyanyasa wamachinga.
Simbachawene alisema hayo wakati
akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam akisema Rais anataka viongozi
na watendaji kuangalia utaratibu mzuri wa kushirikisha wajasiriamali hao ili
kupata ufumbuzi shirikishi zaidi.
“Kwa kuanzia ni vema yakatengwa maeneo
ya katikati ya mji yenye wateja wa bidhaa zinazouzwa, kwa kuangalia uwezekano
wa kufunga mtaa japo mmoja ili utumike kwa kazi za kimachinga,” alisema
Simbachawene.
Alisema usumbufu unaojitokeza maeneo
mbalimbali unasababisha wananchi kupoteza mitaji yao ambayo wengine wamekopa kwenye
vikundi vya vicoba na hivyo kuhatarisha mustakabali wa maisha yao na familia
zao.
Aliongeza kuwa mamlaka zinatakiwa
ziandae maeneo rafiki yenye mahitaji muhimu, ili yaweze kufikika kirahisi na
kuruhusu biashara kufanyika bila shida kabla ya kuhamasisha wafanyabiashara kwa
njia shirikishi zaidi.
0 comments:
Post a Comment