Mwandishi Wetu
VIKAO vya kwanza vya CCM tangu Rais John
Magufuli achaguliwe kuwa Mwenyekiti, vitakavyoanza Jumapili Dar es Salaam, vinatarajiwa
kufanya mabadiliko ya Sekretarieti yake, huku sura kadhaa zikitajwa kuwemo,
JAMBO LEO limedokezwa.
Rais Magufuli ambaye alichaguliwa Julai
23 kuwa Mwenyekiti wa CCM, aliitaka Sekretarieti ya Chama hicho yenye wajumbe wanane
chini na Katibu Mkuu, Abbulrahman Kinana isiondoke, lakini uamuzi wa kuitisha
kikao hicho unaelezwa huenda ukaja na mabadiliko makubwa.
Mabadiliko hayo yanachagizwa zaidi na uteuzi
wa Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho, Rajab Luhwavi kuwa balozi sambamba na Dk
Emmanuel Nchimbi, Dk Pindi Chana na Dk Asha-Rose Migiro ambao walikuwa wajumbe
wa Kamati Kuu. Lakini pia Katibu wa Itikadi an Uenezi, Nape Nnauye ambaye ni
Waziri wa Habari, Sanaa na Michezo.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili, zilieleza
kuwa uteuzi huo ni ishara kwa chama hicho kuanza mchakato wa kusaka makada wengine
wa kuziba nafasi hizo, kama ilivyopata kutokea miaka ya nyuma, hasa wajumbe wa
Sekretarieti walipoteuliwa kuwa mawaziri.
Zilieleza kuwa miongoni mwa watu
wanaoweza kuingia katika Sekretarieti mpya ni pamoja na Waziri wa Ardhi, Nyumba
na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi anayetajwa kwa nafasi ya Katibu Mkuu na Mkuu
wa Mkoa wa Wilaya ya Ubungo Humphrey Polepole, anayetajwa huenda akarithi
mikoba ya Nape.
Wengine ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Amos
Makala na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi, Abdallah Bulembo.
“Unakumbuka Dk Migiro alipovaa viatu vya
January Makamba (Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira na Muungano) kwenye
nafasi ya Katibu wa Siasa na Mambo ya Nje.
“Wakati ule Makamba aliachia nafasi ili
abaki na ya Unaibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia,” kilieleza chanzo
chetu.
Kilifafanua kuwa Dk Migiro baada ya
kuteuliwa kuwa balozi Uingereza, nafasi yake ilikaimiwa na Dk Chana ambaye
ameteuliwa kuwa balozi pia.
“Kwa sasa Nape (Nnauye) ni Katibu wa
Itikadi na Uenezi na pia ni Waziri wa Habari, hivyo inawezekana nafasi yake
ndani ya chama akachukua mtu mwingine. Si ajabu Polepole hata Ole Sendeka
(Christopher) ambaye kwa sasa ni msemaji wa CCM,” alisema mtoa habari huyo.
Taarifa hizo pia zilitolea mfano wa jinsi
Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba alivyoachia mikoba ya Katibu wa NEC
wa Uchumi na Fedha kwa Zakia Meghji, baada ya kuwa waziri.
Katika mabadiliko hayo, taarifa hizo
zinamtaja Lukuvi kuchukua nafasi ya Kinana kutokana na utendaji wake na kuijua
CCM vilivyo licha ya kuwa Katibu Mkuu huyo alichangia kwa kiasi kikubwa
kurejesha nguvu za chama kipindi cha miaka mitano alichoshika nafasi hiyo.
Kinana amekuwa Katibu Mkuu tangu mwaka 2012, akiongoza kampeni ya kuwaaminisha wananchi kuwa CCM ina sera nzuri, huku akishutumu hadharani viongozi wa Serikali kuwa wanakwamisha maendeleo ya nchi.
Wengi wanaamini kuwa kampeni hiyo
ilichangia kuifanya CCM ikabiliane na ongezeko la nguvu ya Upinzani hata
kushinda uchaguzi mkuu uliopita.
Baada ya Rais Magufuli kukabidhiwa uenyekiti wa CCM, aliikubali kazi iliyofanywa na Sekretarieti hiyo na kuitaka iendelee, iwapo ataamua kumpumzisha kwa sasa huenda makada hao wakaula kwa kuzingatia ukada na uzoefu wao.
Lukuvi ni miongoni mwa wanaopewa nafasi
kubwa kutokana na uzoefu wake ndani ya chama, akiwa ameanzia Umoja wa Vijana,
ukuu wa mkoa hadi uwaziri.
Taarifa hizo zinabainisha kuwa Makala ana nafasi kubwa ndani ya chama hicho kwa kuwa alianzia UVCCM hadi kuwa mweka hazina wa CCM na baadaye naibu waziri.
Makala alishindwa kwenye uteuzi wa ubunge wa Mvomero ndani ya CCM na baadaye kuteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro kabla ya kuhamishiwa Mbeya.
“Bulembo naye si mtu wa kubeza kwa sababu anaelewana vema na Rais na pia ana uzoefu ndani ya chama. Kama utakumbuka alikuwa karibu na Magufuli wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita,” zilieleza taarifa hizo.
Wajumbe wa Sekretarieti hiyo iliyo chini
ya Kinana ni Vuai Ali Vuai, ambaye ni Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Luhwavi,
Mohamed Seif Khatib (Katibu wa Oganaizesheni wa Halmashauri Kuu), Migiro,
Meghji na Nape.
0 comments:
Post a Comment