Boeing wakutana na JPM kwa ndege mpya

Mwandishi Wetu

DHAMIRA ya Serikali kununua ndege mpya na kuimarisha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) sasa ni dhahiri kutokana na Rais John Magufuli jana kukutana na Mkurugenzi wa Masoko ya Afrika wa Kampuni ya utengenezaji ndege ya Boeing.

Rais Magufuli alizungumza jana Ikulu, Dar es Salaam na Jim Deboo wea kampuni hiyo yenye makao yake Marekani ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kununua ndege kubwa za kampuni hiyo.

Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa, ilisema mazungumzo hayo yalihudhuriwa na Katibu Mkuu Uchukuzi, Dk Leonard Chamriho na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James.

Baada ya Mazungumzo hayo Rais Magufuli alisema Serikali yake imedhamiria kununua ndege zingine nne zikiwamo kubwa tatu ambazo zitasaidia kuinua uchumi wa nchi kwa kuwezesha watalii kuja nchini moja kwa moja kwao.

"Sisi tunazungumza kuwa watalii hawajafika hata milioni mbili kwa mwaka, lakini nchi ya Morocco inapata watalii zaidi ya milioni 12 kwa mwaka, hii yote ni kwa sababu hatuna mashirika ya ndege ya kwetu.

“Watalii wakitaka kuja hapa ni lazima waje kwa kuungaunga, wafikie nchi nyingine ndipo wapate moyo wa kuja huku, licha ya kwamba sisi ni miongoni mwa nchi tano duniani zenye maeneo mazuri yenye utalii.

"Kwa hiyo niwaombe tu Watanzania wapende mali zao, kwa sababu wakati mwingine nikiangalia mitandao na magazeti, ni ajabu huwezi kuamini kama hao ni Watanzania, wanasifia tu ndege za watu wengine na wanazibeza zao," alisisitiza Rais Magufuli.

Rais alitaja aina ya ndege mpya ambazo Serikali itanunua kuwa ni moja ya Bombardier Q400 Dash 8 NextGen inayotarajiwa kufika nchini Juni mwakani, mbili za Bombardier CS300 zenye uwezo wa kubeba abiria kati ya 137 na 150 na zinazotarajiwa kuwasili nchini kati ya Mei na Juni, 2018.

Pia ndege aina ya Boeing 787 Dash 8 Dream Liner yenye uwezo wa kubeba abiria 262 na inayotarajiwa kuwasili nchini Juni, 2018. Malipo ya awali kwa ndege hizo yameshafanyika.

Dk Magufuli alitaka Watanzania kuunga mkono juhudi hizo zenye lengo la kuinua utalii na kuimarisha uchumi wa nchi.

"Tumeleta ndege aina ya Bombardier, zimepunguza gharama za safari, mfano kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza, sasa wanalipa kati ya Sh 160,000 na Sh 200,000 wakati nauli ilishafika Sh. 800,000 na kitu, lakini watu wengine wanazungumzazungumza wee maneno ya hovyo kwa kutumiwa, tumeshaamua na tutafanya hivyo," alisisitiza Rais.

Wakati huo huo, Rais Magufuli aliagana na aliyekuwa Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika nchini (AfDB) Dk Tonia Kandiero ambaye amepanda cheo na kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Ukanda wa Kusini mwa Afrika katika ofisi zake za Afrika Kusini.

Rais Magufuli alimshukuru Dk Kandiero kwa juhudi kubwa alizofanya nchini ambapo miradi mikubwa na muhimu katika maendeleo imetekelezwa na inaendelea kutekelezwa.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli aliagana na Balozi wa Cuba nchini, Jorge Luis Lopez Tormo anayemaliza muda wake, baada ya kuiwakilisha nchi yake kwa miaka minne.

Rais Magufuli alimshukuru Tormo kwa ushirikiano mzuri aliouendeleza kati ya Tanzania na Cuba uliojengwa na waasisi Baba wa Taifa marehemu Mwalimu Julius Nyerere wa Tanzania na Fidel Castro.

Tormo amemshukuru Rais Magufuli na Serikali kwa kuendeleza   ushirikiano mzuri wa Tanzania na Cuba na kusema anaondoka akiamini kuwa uhusiano wa nchi hizi utaendelea kunufaisha wananchi kupitia miradi mikubwa ya maendeleo na huduma za kijamii.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo